• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
Ruto akaidi NCIC, atoa wimbo wa ‘Sipangwingwi’

Ruto akaidi NCIC, atoa wimbo wa ‘Sipangwingwi’

NA WINNIE ONYANDO

NAIBU wa Rais, William Ruto amekaidi amri ya Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) baada ya kutoa wimbo ambao ameupa jina ‘Hatupangwingwi’, muda wa saa chache baada ya tume hiyo kulipiga marufuku neno hilo.

Siku ya Ijumaa saa tano mchana, Tume ya NCIC iliorodhesha neno hilo kuwa miongoni mwa maneno 23 ambayo yanafaa kuepukika kwa kuwa yanaaminika kuchochea chuki katika kampeni za kisiasa.

Siku iyo hiyo, Dkt Ruto aliutoa wimbo huo ambao alishirikishwa na mwanamuziki Tony Kinyanjui almaarufu E-xray na kuiweka kwenye mtandao wake wa kijamii ya Twitter.

Wimbo huo unatumika na Naibu wa Rais kama kauli mbiu kwenye kampeni zake za kisiasa.

Kwenye wimbo, Dkt Ruto anasikizwa akisema kuwa chama cha United Democratic Alliance (UDA) hakitapangwa kisiasa.

“Kama vile Wakenya wamesema kuwa hawapangwingwi, hata mimi kama ‘hustler’, nasema sipangwingwi,” akasema Dkt Ruto kwenye wimbo huo.

Wafuasi wa Dkt Ruto pia walisema kuwa hawatapangwa na kuwa watalinda kura zao.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa NCIC, Samuel Kobia alisema kuwa maneno kama hayo yamepigwa marufuku kwenye hafla zote a kisiasa zikiwemo kampeni, kwenye mitandao ya kijamii na mazungumzo yoyote ya kisiasa.

“Maneno hayo tuliyoyaorodhesha yatatumika kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Hii itasaidia kupambana na matamshi ya chuki nchini,” akasema Dkt Kobia jijini Nairobi.

Maneno ya Kiingereza yaliyopigwa marufuku na tume hiyo ni Fumigation ambayo inalenga wanajamii ambao si wakazi rasmi wa eneo fulani, Uncircumcised, Eliminate na Kill.

Kwa upande mwingine, maneno ya Kiswahili kama vile Kaffir, Madoadoa, Chunga Kura, Mende, Watu wa kurusha mawe, Watajua hawajui, Wabara waende kwao, Wakuja, Chinja Kaffir na Kwekwe yamepigwa marufuku katika hafla zote za kisiasa.

Maneno ya Kikuyu kama vile Kihii, Uthamaki ni witu hayafai kutamkwa, maneno ya Kimeru kama vile Mwiji na ya Kikalenjin yanayojumuisha Kimurkeldet, Otutu labotonik na Ngetiik yote yamepigwa marufuku.

Maneno Hatupangwingwi, Operashion Linda Kura na Kama noma, noma yote hayafai kutumika.

Kadhalika, tume hiyo pia inamulika vikundi 14 vya mirengo ya kisiasa ya Azimio la Umoja na Kenya Kwanza ambavyo vinaaminiwa kuendeleza matamshi ya chuki uchaguzi wa Agosti 9 ukikaribia.

Vikundi hivyo vinajumuisha Lamu County politics, Migori Revolutionalist Council, The Kalenjin Forum, The New Mamaans Borana, Voices of Change, The Marsabit County We All Want members, The Marsabit County we want, Raila Odinga for President, Group Kericho County, Baba the 5th! Inawezekana. Azimio la Umoja, UasinGishu County Forum, BUNGOMA COUNTY FORUM, Azimio la Umoja na Group Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Malindi Progressive yatamba ikifinyanga vipaji na kukuza...

Mjakazi akiri kumwibia mwajiri tarakilishi

T L