• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
JAMVI LA SIASA: Maasi ya Raila ni ‘moto wa karatasi’

JAMVI LA SIASA: Maasi ya Raila ni ‘moto wa karatasi’

NA BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga anapotarajiwa kuongoza mkutano wa pili wa hadhara jijini Nairobi mwaka huu hivi leo Jumapili katika uwanja wa Jacaranda, kuna hisia kwamba huenda maasi aliyotangaza Jumatatu dhidi ya serikali yakawa moto wa karatasi.

Huku baadhi ya washirika wake wa karibu wakisisitiza kuwa hawatambui William Ruto kama rais wa Kenya na kushikilia kwamba kura za Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9 ziliibwa, kuna wanaouliza maswali kuhusu hatima na manufaa ya maasi aliyotangaza.

Hisia zao ni kwamba Bw Odinga hana mikakati na hata kama ataitisha maandamano kama sehemu ya maasi aliyotangaza Jumatatu wiki hii, hayatachangamkiwa na wafuasi wake ambao baadhi wamekumbatia serikali.

Kuna hisia kwamba maandamano yatasababisha ghasia na kuvuruga biashara jijini ambazo nyingi zinamilikiwa na wafanyabiashara wa eneo la Mlima Kenya.

Wadadisi wanasema ni hisia hizi ambazo zimefanya baadhi ya washirika wake kujitenga na wito wake wa maasi na kuchemkia serikali.

Mnamo Jumatatu, mbunge wa kuteuliwa wa chama cha Jubilee Sabina Chege na mwenzake wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega ambao walipiga jeki kampeni za Bw Odinga Mlima Kenya walikutana na Rais Ruto katika ikulu ya Nairobi kupitia juhudi za Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Ni katibu mkuu wa Jubilee na kiongozi wa chama cha Narc Kenya Martha Karua wanaoonekana kuganda katika Azimio eneo la Mlima Kenya huku baadhi ya wadadisi wakisema Bw Odinga alichelewa kutoa mwelekeo kwa wafuasi wake.

Bw Odinga anategemea ufichuzi unaoashiria kwamba alishinda uchaguzi mkuu wa urais ambao ulianikwa miezi sita baada ya Rais Ruto kuingia mamlakani.

Ufichuzi huo unaodaiwa kutolewa na mfanyakazi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), unaonyesha kuwa Bw Odinga alishinda uchaguzi huo kwa kura 8,170,353 ikiwa ni asilimia 57.3 dhidi ya Dkt William Ruto aliyepata kura 5,915,973 (asilimia 41.66) ya kura za urais wala si kura 7,176,141 (asilimia 50.49 ) za Dkt Ruto dhidi ya 6,942,930 (asilimia 48.5) za Bw Odinga alivyotangaza aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati.

Aliyekuwa ajenti mkuu wa Azimio katika Bomas of Kenya Saitabao Ole Kanchory anaamini kwamba kwa wakati huu Bw Odinga hana mwelekeo wa wazi kwa wafuasi wake.

“Raila Odinga anapaswa kutoa mwelekeo wa wazi. Wakenya hawana muda wa michezo ya kijinga,” Bw Kanchory alisema.

Wakili huyo anasisitiza kuwa ni hatari zaidi kufuata mtu aliyetoa mwelekeo wa wazi kuhusu anakoelekea huku akisisitiza kuwa kura za Bw Odinga ziliibwa.

“Raila Odinga ana chaguo mbili; ya kwanza ni kutuelewa iwapo ana njia ya kutwaa mamlaka. Akituambia ana njia ya kuingia madarakani na atuonyeshe njia ya wazi, nitakuwa wa kwanza kumfuata. Pili anapaswa kutuambia iwapo mpango wake ni kukosoa serikali hii,” Bw Kanchory alisema.

Kulingana na Bw Kanchory kuitisha maasi na kutoa masharti bila njia ya kutwaa mamlaka ni kuharibu wakati wa wafuasi wake.

“Na njia ya kutwaa mamlaka haihusishi kamwe handisheki na Rais Ruto,” asema Kanchory.

Tayari Bw Odinga ametangaza kuwa hatambui Ruto kama rais wa Kenya na yeyote aliye katika serikali yake huku akiitaka kujiuzulu.

Rais Ruto ametaja hatua za Bw Odinga kama vitisho vyake vya kawaida akilenga handisheki na akaonya kuwa hatafaulu.

Bw Kanchory asema kuwa mipango yoyote ya kukosoa serikali lazima iwe thabiti ili iweze kufaulu akiashiria kwamba kufikia sasa Raila hajaonyesha ana mipango kama hiyo.

  • Tags

You can share this post!

WALIOBOBEA: Soita aliifaulisha miradi mingi ya makao katika...

Ruto aokota waliotupwa na Uhuru

T L