• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Ruto asukuma Kingi na Jumwa meza moja

Ruto asukuma Kingi na Jumwa meza moja

GAVANA wa Kilifi, Bw Amason Kingi na mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, Jumatano walikumbwa na changamoto kutuliza wafuasi wao kabla ya Naibu Rais William Ruto kuwasili kwa mikutano ya hadhara Kilifi.

Ilifichuka kuwa, vigogo hao wawili wa siasa za Kilifi walilazimika kuandaa mkutano faraghani mapema asubuhi ili kutatua mizozo yao ya muda mrefu ambayo ilitishia kutatiza ziara ya kampeni za urais ya Dkt Ruto.

Mkutano huo uliohudhuriwa pia na wanasiasa wengine wa vyama vya UDA na PAA, ulimfanya Bw Kingi kuchelewa kuhudhuria kikao kingine cha muungano wao wa Kenya Kwanza katika kaunti jirani ya Mombasa.

“Naomba radhi kwa kuchelewa kuwasili lakini tulikuwa tunaandaa mambo mengine mazuri,” Bw Kingi alisema, alipowasili katika kikao hicho cha Mombasa kikiwa kishaendelea kwa saa kadha.

Baada ya mkutano wa faragha, Bi Jumwa anayewania ugavana Kilifi kupitia kwa UDA, mpinzani wake, Bw George Kithi wa Chama cha PAA, na wanasiasa wengine wa Kenya Kwanza walielekea kwa mkutano wa hadhara ulioonekana kuwa wa kumsafishia njia Dkt Ruto.

Katika mkutano huo uliofanywa uwanjani Msabaha, wanasiasa hao walitatizika kuwashawishi wafuasi wao kutulia kwa maandalizi ya kumwalika kinara wao wa Kenya Kwanza.

Wafuasi wa PAA walizoma viongozi wa UDA, huku wale wa UDA pia wakikataa kuskiza wa PAA.Huku haya yakiendelea, viongozi wa Kenya Kwanza katika kaunti hiyo walitumia mitandao ya kijamii kurai wafuasi wao kuweka kando tofauti zao, angalau mbele za mgeni wao wa heshima ambaye muda wake wa kuwasili ulikuwa unakaribia.

“Ninawaeleza wafuasi wetu kuwa iwapo utakuja katika mkutano, njoo kama mkazi wa Kilifi wala si mwanachama wa UDA au PAA. Usije kuonyesha ubabe, kuzoma na kuzua vurugu bali kuwakilisha Kilifi,” akasema.

Bw Baya amekuwa akisimama na Bi Jumwa kumkemea vikali Bw Kingi kuhusu usimamizi wa kampeni za urais za Dkt Ruto, na kwa kupinga wawaniaji wa UDA anapopigia debe wanachama wa PAA.

Dkt Ruto alifanikiwa kusimamia mkutano wa hadhara bila purukushani nyingi, huku akiongoza wanachama kumpigia debe Bi Jumwa kushinda ugavana mbele ya Bw Kingi, Bw Kithi na wafuasi wa PAA.

Bi Jumwa hakuficha nia yake ya kutaka kuachiwa nafasi ya kupeperusha bendera ya Kenya Kwanza.

“Hii Kilifi hatuwezi kuiacha iende kwa Azimio. Mtafutieni kazi kijana George Kithi na ugavana wa Kilifi ubaki na Aisha Jumwa. Aisha Jumwa ndiye ataweza kupeleka mtu wa Azimio nyumbani. Naomba tena, Kingi anipe kura yake,” akasema.

Kiti hicho kinamezewa mate pia na aliyekuwa waziri msaidizi wa ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro, ambaye ni mwanachama wa ODM.

Ripoti za Maureen Ongala, Valentine Obara na Anthony Kitimo

  • Tags

You can share this post!

Aliyedaiwa kuua mkewe aachwa kwa dhamana

Wanasiasa waombea shida walizochangia kuwaletea Wakenya

T L