• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 8:50 AM
Ruto haonekani kukoma kuvizia wabunge wa upinzani

Ruto haonekani kukoma kuvizia wabunge wa upinzani

NA JUSTUS OCHIENG

KWA mwaka mmoja ambao amekuwa mamlakani, Rais William Ruto ameendeleza mikakati yake ya kuwarai wanasiasa wa upinzani wajiunge na mrengo wake huku akilenga kuongeza uungwaji mkono bungeni na kujiandaa kwa kura ya 2027.

Mara tu baada ya kutangazwa mshindi wa kura za Urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, Rais aliwavizia wanasiasa wa mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya na kusababisha Kenya Kwanza iwe chama chenye wabunge wengi katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

Seneta wa Mandera Ali Roba (UDM) na Mbunge wa Ugenya David Ochieng (MDG) ni kati ya wanasiasa wa kwanza kutoka mrengo wa upinzani ambao walitangaza kuanzisha ushirikiano wa kisiasa na Rais Ruto.

Itakumbukwa kuwa wakati ambapo mjadala ulichacha bungeni kuhusu ni mrengo upi ndio una wabunge wengi, Spika Moses Wetang’ula alitoa uamuzi kuwa Kenya Kwanza ina wabunge 179 huku Azimio la Umoja ikiwa na 157.

Mwanzoni Azimio ilikuwa na wabunge 171 huku Kenya Kwanza ikiwa na 165 lakini hali ikabadilika kutokana na hamahama za wanasiasa wa upinzani hata kabla ya Rais Ruto kuapishwa mnamo Septemba 15.

Kuwa na idadi kuu ya wabunge kumemsaidia Rais Ruto kupitisha miswada mbalimbali ikiwemo ule uliopingwa vikali na upinzani, Mswada wa Fedha 2023, ambao sasa ni sheria.

Hatua ya Rais Ruto kuwaleta wabunge wa upinzani kambini mwake kunalenga kumsaidia kurejea mamlakani mnamo 2027 bila kutolewa jasho. Ingawa hivyo, nia yake ya kuvivunja vyama tanzu ndani ya Kenya Kwanza imepingwa hasa na vyama vya Ford Kenya na ANC vinavyoongozwa na Bw Wetang’ula na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi.

Chama pekee ambacho kilivunjwa ni kile cha Waziri wa Biashara Moses Kuria ambaye alitangaza kuwa sasa amejiunga na UDA.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa ambaye ni wa UDA ni kati ya wabunge ambao wanapinga vyama tanzu kuvunjwa na kujiunga na UDA. Barasa anasema vyama hivyo vidogo vinastahili kuheshimiwa hasa na UDA.

“Tulipohitaji kuwa na idadi ya juu ya wabunge, ni vyama hivi vidogo ambavyo Katibu wa UDA Cleophas Malala alivirejelea kama vyama vya vijiji ndivyo vilitusaidia. Tuheshimu vyama vyote badala ya kuvilazimisha vivunjwe,” akasema Bw Barasa.

Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi naye anasema hatua ya Rais Ruto kuwachukua baadhi ya wabunge wa upinzani ni kuhujumu demokrasia na si nia nzuri wakati mazungumzo ya kupatanisha upinzani na serikali yanaendelea.

Wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu) na Jaheer Jhanda (Nyaribari Chache) nao wanasema utendakazi wa Rais Ruto kwenye mwaka wake wa kwanza wa uongozi ni wa kupigiwa mfano.

  • Tags

You can share this post!

Vifaabebe kwa watoto wachanga huwacheleweshea uwezo wa...

Hofu wanaougua ukoma wakiendea wapiga ramli kwa kuamini ni...

T L