• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
Hofu wanaougua ukoma wakiendea wapiga ramli kwa kuamini ni maradhi ya laana

Hofu wanaougua ukoma wakiendea wapiga ramli kwa kuamini ni maradhi ya laana

NA SIAGO CECE

MAAFISA wa afya wameshikwa na hofu huku wakazi wa Kwale wanaougua ugonjwa wa ukoma wakianza kutafuta usaidizi wa wapiga ramli na waganga wa tiba za kienyeji kwa matibabu.

Wakati huo huo, kaunti hiyo inakosa wahudumu wa kutosha wa kutibu ugonjwa huo.

Haya yanajiri wakati ripoti ya hivi majuzi ya wizara ya afya kusema kuwa visa vya ukoma 120 viliripotiwa nchini mwaka 2022, huku watu 21 wakiugua katika Kaunti ya Kwale.

Waziri wa Afya wa Kaunti ya Kwale Francis Gwama alisema ukosefu wa ufadhili wa kutosha unazuia juhudi za kuwahamasisha wahudumu.

Afisa huyo alisema wagonjwa wa ukoma wanatafuta matibabu kutoka kwa waganga wakiamini ugonjwa huo unatokana na laana au uchawi.

“Wagonjwa wa ukoma hawaji hospitalini kwa sababu ya kutokuwa na ufahamu na hivyo kuwalazimu kutafuta matibabu kutoka kwa waganga na kwa bahati mbaya kufika hospitalini kuchelewa,” alisema.

Bw Gwawa alisema uhaba wa fedha pia unazuia kugundulika kwa ugonjwa huo mapema.

“Ikiwa kesi mpya inaripotiwa, huwa tunatakikana kutuma mhudumu wa afya kwa familia ili kuona kama kuna wanajamii wengine wanaoonyesha dalili lakini kwa vile hatuna ufadhili, hii haifanyiki,” Bw Gwama alisema.

Alisema kwa sasa wanaotibiwa katika Hospitali ya Msambweni ambayo ina kitengo halisi cha ukoma, ndiyo wagonjwa pekee wanaofika hospitalini hapo, lakini hakuna ufuatiliaji unaofanyika hivyo kuonyesha namna kuna changamoto kubwa katika jamii.

Bw Gwama aliwataka wakazi kutafuta usaidizi kutoka kwa hospitali hiyo wanapogundua au kuonyesha dalili hizo.

Mwanaulu Ali, ambaye ni mkazi aliyekuwa akiugua ugonjwa wa ukoma na kupata matibabu, alisema bado watu wengi hawana ufahamu wa ugonjwa huo huku wengi wa wagonjwa hao wakipelekwa kwa waganga kwa matibabu wakiamini kuwa ni uchawi.

“Wazazi wangu waliamini tulirogwa mara ya kwanza walipogundua kuwa mimi na kaka yangu tulikuwa tunaugua ukoma. Baadaye tuliletwa hospitalini hapa Msambweni na tukapona,” akasema Bi Ali ambaye sasa anaishi katika kijiji cha Tumbe, Msambweni, Kaunti ya Kwale.

Yeye ni miongoni mwa walionufaika na kituo cha zamani cha matibabu ya ukoma kilichokuwa kikitoa matibabu ya bure kwa wagonjwa wote walioripotiwa Kwale hadi hospitali ilipofungwa na kugeuzwa tawi la Kenya Medical Training College (KMTC) Msambweni.

Haya yanajiri huku kukiwa na wasiwasi kwamba huenda Kenya ikapoteza mafanikio ambayo yamesababisha ugonjwa huo kutangazwa kufifia na Shirika la Afya Duniani (WHO) ikiwa matibabu ya ugonjwa huo hayatafanyika.

  • Tags

You can share this post!

Ruto haonekani kukoma kuvizia wabunge wa upinzani

Mitandao iwe ya kupeana habari na sio kushambuliana,...

T L