• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:36 PM
Ruto kufufua BBI kubuni vyeo zaidi

Ruto kufufua BBI kubuni vyeo zaidi

NA LEONARD ONYANGO

NAIBU Rais William Ruto ataleta baadhi ya mabadiliko katika serikali yake iwapo atashinda urais, sawa na yaliyopendekezwa na Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga kwenye BBI.

Hii ni kinaya kwa kuwa Dkt Ruto alikuwa mkosoaji mkubwa wa BBI akidai kuwa lengo lake lilikuwa kubuni vyeo kwa masilahi ya viongozi wachache, na hivyo kuumiza raia kwa ushuru wa juu kulipa mishahara.

Kulingana na mkataba wa ugawanaji madaraka aliotia sahihi mnamo Aprili 5 na Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, pamoja na mwenzake wa Ford-Kenya, Moses Wetang’ula, serikali ya Kenya kwanza itabuni ofisi ya waziri mkuu mwenye mamlaka makubwa hata kuliko yaliyokuwa yamependekezwa katika BBI.

Kinyume na utaratibu waliokuwa wametumia Rais Kenyatta na Bw Odinga, Serikali ya Dkt Ruto itatumia bunge kubuni wadhifa wa waziri mkuu ndani ya siku 14 baada yake ‘kuapishwa kuwa rais’.

Jina la mtu atakayekuwa waziri mkuu litapendekezwa na ANC kisha atateuliwa rasmi na Dkt Ruto.

Serikali ya Kenya Kwanza pia itawasilisha Bungeni mswada wa sheria itakayotoa mwongozo kuhusu majukumu ya waziri mkuu ndani ya siku 30 baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

“Rais atateua mtu huyo kuwa waziri mkuu bila pingamizi. Akiwa rais, Dkt Ruto atatumia mamlaka yake kutangaza majukumu ya waziri mkuu kupitia Gazeti Rasmi la Serikali,” unasema mkataba huo.

Mamlaka ya waziri mkuu yatakuwa kusimamia wizara za serikali, utekelezwaji wa sera za serikali na pia wizara ya usalama itakuwa chini yake.

Waziri Mkuu pia atasimamia shughuli zote za miswada ya serikali inayowasilishwa Bungeni na kutathmini sera na miradi ya serikali.

Majukumu ya waziri mkuu katika Mswada wa BBI yalikuwa kusimamia shughuli za serikali bungeni na utendakazi wa idara za serikali pekee.

Tofauti na Mswada wa BBI uliopendekeza kuwa ni sharti waziri mkuu awe mbunge, mkataba wa Kenya Kwanza hauzingatii hilo.

Kwenye mkataba huo, waziri mkuu anaonekana kuwa na mamlaka makubwa kuliko naibu rais ambaye majukumu yake yatakuwa kuongoza kamati za mawaziri, kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya baraza la mawaziri, kudumisha uhusiano baina ya serikali kuu na kaunti, kusimamia miradi ya serikali na kushirikiana na tume na taasisi huru.

Mara baada ya kuapishwa, Dkt Ruto anasema atatumia mamlaka yake kuchapisha katika Gazeti Rasmi la Serikali majukumu ya Naibu wa Rais ili kuepuka ‘kuhangaishwa na rais kama ilivyomtendekea’.

Mkataba huo unaeleza kuwa chama cha UDA kitatoa rais pamoja na naibu wake. Hii inaonyesha kuwa wadhifa wa naibu rais umetengewa eneo la Mlima Kenya.

Chini ya mkataba huo, chama cha Ford Kenya kitatoa jina la mtu atakayekuwa spika wa Bunge la Kitaifa.

Pia vyama vya ANC na Ford Kenya kwa pamoja vitatengewa asilimia 30 ya nyadhifa serikalini zikiwemo za mawaziri, makatibu wa wizara, mabalozi, wenyeviti wa mashirika ya serikali, wakurugenzi wa mashirika ya umma na tume huru. Pia vitateua kiranja wa wabunge wa muungano wa Kenya Kwanza.

“Nyadhifa za uanachama haswa uenyekiti wa kamati za Bunge zitatolewa kwa kuzingatia idadi ya wabunge au maseneta ambao kila chama kimeshinda. Kanuni sawa na hiyo itazingatiwa katika mabunge ya kaunti,” unasema mkataba huo.

Sharti ambalo limewekwa ni kuwa vyama vya ANC na Ford Kenya visaidie Dkt Ruto kufanya kampeni kote nchini.

Mkataba huo pia unaahidi kuwa serikali itakamilisha miradi yote ya barabara inayoendelea katika eneo la Magharibi ambalo ni ngome ya ANC na Ford Kenya kwa kujenga barabara mpya za urefu wa kilomita 1,000 za lami.Mkataba huo pia unasema serikali ya Kenya Kwanza itafufua viwanda vya sukari kama vile Nzoia na Mumias na kujenga viwanda vya samaki kati ya miradi mingineyo.

  • Tags

You can share this post!

Pensheni: Wabunge wataka donge nono tena

Mahakama yazuia IEBC kuidhinisha Sonko kushiriki uchaguzi...

T L