• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 7:55 PM
Sina ubaya na Rais Kenyatta, asema Dkt Ruto

Sina ubaya na Rais Kenyatta, asema Dkt Ruto

NA SAMMY WAWERU

RAIS mteule William Ruto ameahidi kuzungumza na Rais anayeondoka, Uhuru Kenyatta kuhusu mchakato wa kupokezwa mamlaka.

Dkt Ruto ametoa tangazo hilo Jumatatu, kwenye hotuba yake kwa taifa baada ya Mahakama ya Upeo kuidhinisha ushindi wake ilipotupa kesi ya kinara wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga aliyekuwa amepinga matokeo ya kura za urais. Wapigakura nchini Kenya walipata fursa ya kumchagua Rais kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Rais Kenyatta alikuwa anampigia debe Raila Odinga amrithi akimtaja Dkt Ruto kama kiongozi mnafiki na ambaye hajakomaa kuiongoza nchi.

“Nitampigia simu Rais Kenyatta. Hatujazungumza kwa muda wa miezi kadhaa. Tutajadiliana kuhusu mikakati ya mimi kupokezwa madaraka inavyotakikana Kikatiba,” akasema Dkt Ruto.

Rais Kenyatta na Dkt Ruto (aliyehudumu kama naibu wa rais 2013 –2022), wamekuwa wakitofautiana hadharani hasa baada ya kiongozi huyo wa nchi anayeondoka na kiongozi wa ODM, Raila Odinga kutangaza kuzika tofauti zao za kisiasa kupitia salamu za maridhiano, Handisheki mnamo Machi 09, 2018.

Licha ya tofauti zao, Dkt Ruto amesema hana uhasama wowote ule na Rais huyo anayeondoka.

“Ninajua alifanya bidii kivyake, ila Wakenya walifanya uamuzi. Tunaishi katika nchi inayothamini demokrasia. Nilipomuunga mkono, sikuweka vikwazo vyovyote. Sina uhasama wowote kwa sababu ya uamuzi wake kuunga mwingine. Tutasalia kuwa marafiki. Tutamheshimu kama rais mstaafu,” akaahidi.

Dkt Ruto anatarajiwa kuapishwa rasmi kama Rais wa Tano wa Jamhuri ya Kenya, siku saba baada ya Mahakama ya Upeo kutoa maamuzi. Hii ina maana ataapishwa rasmi Septemba 13, 2022.

  • Tags

You can share this post!

Ruto asema serikali yake itajenga mazingira mazuri kwa...

Kiraitu sasa adai Munya ndiye alichangia kushindwa kwake na...

T L