• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 7:55 AM
Uhuru achemka kwa kuhepwa ngome yake

Uhuru achemka kwa kuhepwa ngome yake

NA MWANGI MURURI

RAIS Uhuru Kenyatta ameripotiwa kukasirishwa na washauri wake kuhusu ripoti zao za hali ya kisiasa katika eneo la Mlima Kenya.

Hii ni baada ya wanasiasa tajika kutoka kaunti yake ya Kiambu kujiunga na mrengo wa Naibu Rais William Ruto mnamo Jumapili, siku moja tu baada ya Rais Kenyatta kumwidhinisha Raila Odinga kuwania urais Agosti 9.

Waliomhepa rais Jumapili ni Kiranja wa Wengi katika Seneti Kimani wa Matangi, aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo, Mbunge wa Thika Mjini Wainaina wa Jungle, Spika wa Kaunti ya Kiambu Stephen Ndichu, aliyekuwa mbunge wa Ruiru Esther Gathogo na madiwani 30 wa Kiambu.

Wengine ambao wamehama majuzi na kujiunga na Dkt Ruto ni Seneta wa Embu Njeru Ndwiga, Mbunge wa Maragua Mary wa Maua, Gavana wa Tharaka Nithi Muthomi Njuki na mwenzake wa Nyeri Mutahi Kahiga.

Duru zilieleza Taifa Leo kuwa rais amewapa wiki moja wandani wake kumpatia ripoti ya hali halisi ya siasa katika eneo la Mlima Kenya.

Maafisa hao ni pamoja na Katibu wa Wizara wa Usalama wa Ndani Karanja Kibicho, Mratibu wa siasa katika Jubilee Nancy Gitau, mkuu wa idara ya Ujasusi Wachira Kameru, Mkurugenzi wa DCI George Kinoti na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni.

UTAWALA WA MIKOA

Maafisa wa utawala wa mikoa waliozungumza na Taifa Leo jana Jumatatu, wakiwemo machifu, makamishna na manaibu wao walisema wameagizwa kuandaa ripoti ya hali halisi na jinsi mradi wa Azimio unavyopokelewa na wakazi mashinani.

“Rais hajafurahia matukio ya hivi karibuni kuhusu uasi ambao amepata kutoka kwa wanasiasa hasa wale kutoka Kiambu. Amefoka sana kuhusu aibu inayomkumba na ametaka jibu kuhusu ni kwa nini hali hiyo haikudhibitiwa kabla yake kumwidhinisha Bw Odinga mnamo Jumamosi,” akafichua mmoja wa wandani wa Rais.

Lakini Bw Kioni alionekana kupuzilia mbali athari za waliohama kwa hesabu zao kuhusu Azimio.

“Tuko na mbinu ya kuziba mianya inayoachwa na wanaotuhama. Isisahaulike kwamba Rais Kenyatta ana tajiriba ya kuwa nje na ndani ya serikali. Amehudumu kama kinara wa upinzani na pia kinara wa serikali. Haya ni mambo madogo ambayo atatumia busara kurekebisha,” akasema Bw Kioni.

Wandani wa Dkt Ruto nao walionekana kushabikia kile walichosema ni ‘kuaibishwa’ kwa rais nyumbani kwake.

“Haya ni matokeo ya kupewa habari za uwongo na wandani wake. Wamekuwa wakimdanganya Uhuru kwamba hali iko sawa huku wakitisha wanasiasa walio na imani kwa Ruto kwamba wajiunge na Azimio la sivyo watatafutiwa makosa na washtakiwe,” akadai mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua.

Akihamia mrengo wa Dkt Ruto, Bw Wamatangi alisema alichukua hatua hiyo kutokana na hali ilivyo mashinani.

USHAWISHI

“Mimi nimezunguka katika Kaunti ya Kiambu nikikusanya maoni ya wananchi na pia mwongozo wa kisiasa, na kwa kauli moja nimeambiwa hata na familia yangu kwamba afueni yangu imo UDA,” akasema Bw Wamatangi akiwa Thika.

“Nimeshangaa kuwa katika mikutano ya Ikulu tumekuwa tukiambiwa kwamba hali ni tofauti mashinani. Tumekuwa tukiambiwa rais wetu bado ana ushwawishi. Lakini kuna ushahidi kwamba hali hiyo sio sahihi,” akasema Bw Ndichu.

Seneta Ndwiga jana Jumatatu alisema aliamua kuhamia UDA baada ya kutambua wakazi wengi wa Mlima Kenya wanaegemea UDA.

“Wakazi wengi wamo UDA. Hivyo siwezi kufanya kosa la kutetea kiti changu kwa tiketi ya Jubilee ambayo umaarufu wake umedidimia,” akaeleza Bw Ndwiga.

Awali waliokuwa wakereketwa wa Rais Kenyatta wakiongozwa na Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru walihamia UDA.

Lakini Bw Kioni alishikilia kuwa Rais Kenyatta bado ndiye simba wa siasa za Mlima Kenya, na nia yake ya kumsaidia Bw Odinga kumzuia Dkt Ruto kutwaa urais itatimia.

KUCHAFUA SIFA

Kulingana na Mwakilishi wa Wanawake wa Nyandarua, Faith Gitau, juhudi za kuuza Azimio eneo la Mlima Kenya zinakumbwa na pingamizi kutokana na matukio ya awali, ambapo Rais Kenyatta mwenyewe aliongoza kampeni ya kumchafulia jina Bw Odinga wakati wa kampeni za 2013 na 2017.

Anasema kwa upande mwingine wakazi wanahisi kuwa Dkt Ruto anastahili ufuasi wao kutokana na mchango wake katika kuchaguliwa kwa Rais Kenyatta mnamo 2013 na 2017.

“Dkt Ruto alitusaidia kutwaa urais 2013 na 2017. Ndiposa tunahisi kuwa ni usaliti mkubwa kumgeuka aliyetufaa ‘wakati wa shida’ na kusimama nasi,” asema Bi Gitau.

You can share this post!

Mututho sasa amezea mate useneta kaunti ya Nakuru

Wajumbe 5,000 wa UDA kumwidhinisha Ruto leo

T L