• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Urais: Midahalo ya wawaniaji wenza wa mirengo tofauti itafanyika Julai 19

Urais: Midahalo ya wawaniaji wenza wa mirengo tofauti itafanyika Julai 19

NA CHARLES WASONGA

MIDAHALO kati ya wagombea wenza kwenye kinyang’anyiro cha urais itafanyika Jumanne, Julai 19, 2022, katika Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afrika Mashariki (CUEA) mtaani, Karen, Nairobi.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumatano, sekritariati inayoongoza Midahalo ya Urais, ilisema kuwa midahalo hiyo itaendeshwa kwa makundi mawili, kwa misingi ya umaarufu wa wagombea wenza hao.

Mdahalo wa kwanza utashirikisha wagombea wenza ambao umaarufu wa hivi punde ni chini ya asilimia tano (5). Wao ni Bi Justina Wamae, ambaye ni mgombea mwenza wa Profesa George Wajackoyah wa chama cha Roots na Bi Ruth Mutua ambaye ni naibu wa mgombea urais wa chama cha Agano David Mwaure Waihiga.

Mdahalo wa pili utashirikisha wagombea wenza ambao umaarufu wao umezidi asilimia tano (5) katika kura ya maoni ambazo zimefanyika katika siku za hivi karibuni.

Wao ni; Bi Martha Karua ambaye ni mgombea mwenza wa Raila Odinga (Azimio la Umoja One Kenya) na Rigathi Gachagua ambaye ni mgombea mwenza wa Naibu Rais William Ruto (chama cha United Democratic Alliance-UDA).

“Kwa mara nyingine tunakariri kujitolea kwetu kuendesha mdahalo ambao utazingatia haki, maadili, huru na uwajibikaji ilivyoelezwa katika Mwongozo wa Midahalo ya Urais,” sekritariati hiyo ikasema kwenye taarifa hiyo.

Midahalo hiyo miwili itaelekezwa na wanahabari kutoka runinga za KBC, NTV, KTN, Citizen na TV47.

Kulingana na taarifa hiyo, Linda Alela wa TV47 na Jacob Kioria wa KBC ndio wataelekeza mdahalo wa kwanza huku Sophia Wanuna wa KTN na John Smart wa NTV wataelekeza mdahalo wa awamu ya pili.

Mdahalo wa kwanza utafanyika kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa moja na nusu usiku huku ule wa pili ukiendeshwa kuanzia saa mbili za usiku hadi saa nne usiku.

“Waelekezi wa midahalo wameteuliwa kwa kuzingatia vigezo vilivyokubalika na ni wataalamu ambao hawatapendelea upande wowote. Aidha, waelekezi na wanahabari wenye uelewa mpana wa siasa nchini na masuala muhimu ya uchaguzi,” sekritariati hiyo ikasema.

Mkuu wa Sekritariati hiyo ni Mkuu wa Idara ya Uhusiano Mwema katika Shirika la Habari la Nation (NMG) Clifford Machoka.

Matokeo ya kura za maoni za hivi punde yanaonyesha kuwa mgombeaji wa urais wa Azimio Raila Odinga ndiye anashabikiwa na wapiga kura wengi akifuatia na Dkt William Ruto wa UDA.

Kwa mfano, katika matokeo ya utafiki uliotolewa na kampuni ya Infotrak Bw Odinga anaongoza kwa umaarufu wa kiwango cha asilimia 43 huku akifuatwa kwa Dkt Ruto kwa asilimia 37. Naye Profesa Wajackoyah ana umaarufu wa asilimia 5 huku Bw Waihiga akikosa kufikisha umaarufu wa chini ya asilimia moja.

You can share this post!

IEBC yasema imeweka mikakati ya kuzuia changamoto katika...

Tolgos atetea umaarufu wa Raila Rift Valley

T L