• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 5:46 PM
Miungano yatishia usalama kwa uvumi

Miungano yatishia usalama kwa uvumi

LEONARD ONYANGO NA JUMA NAMLOLA

ZIKIWA zimesalia siku sita pekee kabla Uchaguzi Mkuu hapo Jumanne ijayo, wanasiasa kwenye mirengo mikuu ya Kenya Kwanza na Azimio wamegeukia kueneza uvumi usio na msingi katika juhudi za kusaka kura, lakini wakati huo huo kuchochea wafuasi wao.

Wachanganuzi wa siasa wanasema wanasiasa wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais Dkt William Ruto na mwaniaji urais wa Azimio Raila Odinga wamegeukia uvumi baada ya kuishiwa na mawazo kuhusu sera ambazo wanashikilia.

Mdadisi wa siasa Javas Bigambo anasema ukosefu wa manifesto thabiti ya kushawishi wapigakura ndio unasababisha wanasiasa kukumbatia uvumi kwa lengo la kuibua hisia na kujipatia kura.

“Kwa mfano, madai ya Ruto na Gachagua kuwa rais analenga kuwaua ni ujanja wa kuibua hisia ili wapigiwe kura. Hata wao wanajua kuwa wanasema uongo. Propaganda huwa jambo la kawaida siku ya uchaguzi inapokaribia. Lakini propaganda hizo zinaweza kuwa hatari kwani zinasababisha uhasama na hata kuchochea machafuko wakati na baada ya uchaguzi,” anasema Bw Bigambo.

Mdadisi mwingine, Michael Agwanda kwa upande wake anasema kuwa Dkt Ruto na Bw Odinga ndio wanafaa kulaumiwa kwa kuruhusu washirika wao kuleta taharuki ya kisiasa nchini huku wakishabikia.

“Viongozi wa Azimio la Umoja na Kenya Kwanza wameacha kuelezea wapigakura mipango yao ya maendeleo. Badala yake sasa wanashambuliana wao wenyewe kibinafsi. Wawaniaji wa viti vidogo kama vile udiwani, ubunge na ugavana pia wanaiga viongozi hao na wanaendeleza chuki mashinani. Hiyo ni hatari kwani jumbe hizo za kupotosha zinaweza kuleta mapigano nchini,” asema Bw Agwanda.

Msemaji wa Serikali Cyrus Oguna pia ametahadharisha kuhusu uvumi ambao umekuwa ukienezwa na mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio, akisema inaweza kuchochea wafuasi wao kufanya ghasia.

Baadhi ya jumbe zenye uvumi ambazo zimekuwa zikienezwa zinalenga kuzua shaka kuhusu kuwepo kwa uchaguzi wa kweli na haki, jambo ambalo wadadisi wanaeleza lina uwezo wa kuchochea ghasia watakaoshindwa wakidai kuwepo kwa udanganyifu.

WIZI WA KURA

Wiki mbili zilizopita kulizuka uvumi kuwahusu raia watatu wa Venezuela waliodaiwa kuingiza vifaa vya kura nchini kwa njia haramu.

Wakati huo, idara ya polisi ikiongozwa na Inspekta Jenerali Hillary Mutyambai na Mkurugenzi wa DCI George Kinoti ilidai huenda kulikuwa na njama za kuiba kura, lakini baadaye walikutana na Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati na kutangaza kuwa walisuluhisha jambo hilo.

Madai hayo ya wizi wa kura yalizidi pale iliposemekana kuwa huenda mrengo wa Kenya Kwanza ulikuwa umeunda njama ya kuiba kura kupitia Uganda.

Kenya Kwanza nao waliwakemea machifu na kudai kuwa wanatumiwa na mawaziri Fred Matiangi (Usalama) na Joe Mucheru (Mawasiliano) kuiba kura kwa niaba ya mwaniaji wa Azimio, Raila Odinga.

Kenya Kwanza pia wamekuwa wakisambaza uvumi kuwa Bw Odinga atamaliza Ukristo akishinda urais.

Waziri Raphael Tuju na mgombea mwenza wa urais wa Azimio, Martha Karua nao wameeneza uvumi kuwa Mlima Kenya hauna deni lolote na Dkt Ruto, kwa kuwa ‘alilipwa’ kumuunga mkono Rais Kenyatta mnamo 2013.

“Mtu ambaye alinunuliwa ili amuunge mkono rais hawezi kutuambia kuwa ana deni na jamii nzima,” akasema Bw Tuju huku akidai kuwa na ushahidi anaoweza kuwasilisha kortini akihitajika.

Wiki hiyo hiyo, Rais Uhuru Kenyatta alikuwa na mkutano wa faragha na viongozi jijini Nakuru ambapo baadaye Dkt Ruto alidai kuna njama ya rais kumuua yeye na watoto wake.

Rais Kenyatta hata hivyo alipuuza madai hayo.

Rais Kenyatta pia amekuwa akidai kuwa mrengo wa Kenya Kwanza unaongozwa na wafisadi bila kutoa ushahidi wowote kuhusu madai yake.

Madai hayo ya Rais Kenyatta pia yanazua maswali kuhusu alichofanya katika utawala wake wa miaka 10 kukabiliana na ufisadi kama kweli alijua watu waliokuwa katika serikali yake walikuwa wakiiba.

Madai ya punde zaidi ni ya Jumatatu akiwa mjini Eldoret, ambapo Dkt Ruto alidai kuzuiwa kuingia eneo la Nyanza na Bw Odinga, kwa kuwa anaogopa: “Bwana….amefunga njia zote za kuingia Nyanza kutumia mawe na majabali. Anaogopa watu wa Nyanza watanunua sera zetu…”

Madai haya kulingana na wachanganuzi, ni mojawapo ya mbinu chafu zinazotumiwa na wanasiasa dakika za mwisho ili kuwavutia wapigakura ambao huenda hawajafanya uamuzi.

  • Tags

You can share this post!

Magoha ashangaza kufunga shule ghafla

MUME KIGONGO: Usipolala vizuri mbegu za kiume zitapungua

T L