• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
DCI yapaka tope IEBC kura ikibisha

DCI yapaka tope IEBC kura ikibisha

NA JUMA NAMLOLA

IDARA ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) imeendelea kuipaka tope Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) zikiwa zimebaki siku 14 pekee Uchaguzi Mkuu kuandaliwa Agosti 9.

Kwenye barua ya kurasa 11 jana Jumapili, Mkurugenzi wa DCI George Kinoti anazua shaka kuhusu kutegemewa kwa IEBC kuandaa uchaguzi huru na wa haki.

Bw Kinoti anamwonyesha Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati kama aliye kwenye njama ya kukoroga uchaguzi.

Katika tukio lililozua maswali zaidi kuhusu nia ya Bw Kinoti, maafisa wa DCI walivamia ofisi inayomilikiwa na mwaniaji urais wa Kenya Kwanza, William Ruto katika Jumba la Transnational jijini Nairobi kwa kile walisema ni kuchunguza habari fulani katika ofisi hiyo.

Uvamizi huo ulifanywa saa chache baada ya Dkt Ruto kumkashifu Bw Kinoti akimtaka akome kuingilia kazi ya IEBC.

Wachanganuzi wa siasa wanasema matukio yanayoendelea ni sawa na ya chaguzi zilizopita ambapo upande mmoja kwenye kinyang’anyiro hufanya kampeni ya kuzua shaka kuhusu uwezo wa IEBC kuandaa uchaguzi wa kuaminika.

Kulingana na Bw Kinoti, sakata ya sasa ilianza Alhamisi wakati raia wa Venezuela, Jose Gregorio Camargo Castellanos alipokamatwa akitoka Panama kupitia Uturuki, maafisa wa usalama katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta walipoona walivyoshuku kwenye mkoba wake.

Alipotakiwa kuufungua, mlipatikana vifaa vya uchaguzi vya kaunti 11.

“Vifaa hivyo vya uchaguzi vilikuwa vya Nairobi (3), Kiambu (2), Nakuru (2) na Meru (2). Kaunti za Machakos, Murang’a, Bomet, Nyeri, Tharaka Nithi, Nyandarua na Kericho vilikuwa na kimoja kimoja. Pia kulikuwa na furushi moja ambalo halikuwa limeandikwa ni la kaunti gani,” ikasema taarifa ya DCI.

Kwenye mkoba wa pili, polisi wasema walipata laptopu, flashi, simu na vifaa vingine vya kutumika na kompyuta.

“Alipohojiwa, alikiri kuwa vifaa hivyo vilikuwa mali yake na kamwe si vya IEBC… Maafisa wetu walimkamata na akadai kuwa alipewa vifaa hivyo na kampuni ya M/S Smartmatic International Holding B.V ili aviwasilishe kwa afisi ya Abdulahi Abdi Mohamed jijini Nairobi,” ikasema taarifa hiyo.

DCI inasema kulingana na Kifungu cha 46(1) cha Sheria za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu mizigo, mshukiwa Jose Gregorio Camargo Castellanos alipaswa kujaza fomu F-88 katika afisi ya forodha.

KUKAMATWA

Kulingana na barua hiyo, mgeni huyo alialikwa na kutafutiwa visa na Bw Abdi, na wala si IEBC.

Alipokuwa akihojiwa, raia wawili wa Venezuela Joel Gustavo Rodriguez na Salvador Javier Suarez walifika uwanjani na kumwulizia.

“Walikamatwa na ikabainika walikuwa wameingia nchini wakitumia pasipoti ambazo muda wake uliisha. Wao pia walikuwa na vifaa 17 walivyopeleka kwa afisi za Abdulahi Abdi Mohamed. Walikamatwa na kupelekwa makao makuu ya polisi wa kupambana na ugaidi (ATPU). Polisi walikagua walikokuwa wakikaa na wakapata kompyuta na flashi zilizopelekwa kwa ukaguzi….Kufikia sasa vifaa 17 walivyoingia navyo washukiwa wa kwanza havijulikani viliko, isipokuwa kama Bw Chebukati atawaeleza Wakenya, kwa kuwa hajalalama kuvuhusu,” ikaendelea kueleza taarifa ya DCI.

Walipokamatwa Ijumaa, Mwenyekiti wa IEBC Bw Wafula Chebukati aliandika barua ya kulalama kwamba wafanyikazi wa kampuni inayoshirikiana na tume yake walikuwa wamekamatwa na kupokonywa vifaa muhimu vitakavyotumika uchaguzini.

DCI inasema kama kweli IEBC iliipa kandarasi Smartmatic International Holding B.V kuwasilisha vifaa vya uchaguzi, mshukiwa alipaswa kuwasiliana moja kwa moja na IEBC na wala si kupitia kampuni inayojulikana kama Seamless Limited.

Isitoshe, kulingana na polisi, Bw Chebukati na Bw Abdi inaonekana hawakuwa na habari kuhusu vifaa alivyokuwa amebeba mshukiwa.

“Jamaa huyo alipokamatwa, Bw Chebukati alidai polisi walimkamata mfanyikazi wa IEBC bila hatia… inaonekana nia yake ilikuwa kuwatia presha maafisa wa usalama kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, ili waachane na uchunguzi,” inasema taarifa hiyo.

Sasa Bw Kinoti anamtaka Bw Chebukati ajitokeze na kueleza Wakenya kuhusu kisanga hicho, na kama atakuwa na ushahidi auweke hadharani kwamba washukiwa walikuwa na nia njema kwa Kenya.

Hapo jana Jumapili ofisi ya habari ya IEBC ilisisitiza kuwa msimamo wa awali wa Bw Chebukati ndio wa kweli.

  • Tags

You can share this post!

Wagombea urais waingia baridi kuhusu mdahalo

Wake wa vigogo wajitosa kupigia debe mirengo yao

T L