• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Vijana waliozoea kula vya haramu kwa uhalifu wasema ukusanyaji taka umefanya jamii kuwakubali

Vijana waliozoea kula vya haramu kwa uhalifu wasema ukusanyaji taka umefanya jamii kuwakubali

NA FRIDAH OKACHI

VIJANA wanne kwenye kundi linalojiita ‘Kifagio’ wamenufaika na mradi wa kuokota taka.

Vijana hao ambao shughuli zao ziko katika maeneo ya Kikuyu na Dagoretti, wamepata pikipiki, Tuk-tuk na biashara ya kuuza viatu.

Kundi la Kifagio linajumlisha vijana 32 wa umri kati ya miaka 18 hadi 35, baadhi yao zamani wakijihusisha na uhalifu lakini sasa wamechukua mkondo mzuri wa maisha.

Kwenye kundi hilo, vijana watatu wamenufaika na kufanikiwa kufungua biashara zao.

Mwaka 2024 kundi hilo lina maono ya kushikana na kumsaidia kijana mwingine kufanikisha ndoto yake ya kupata gari la kufanyia biashara ya teksi kupitia apu ya Uber.

Adams Kihure Mwangi sasa anatumia Tuktuk yake kwa shughuli za biashara ya kunadi bidhaa zake baina ya Loitoktok na Limuru.

Adams Kihure Mwangi sasa anatumia Tuktuk kwa shughuli za kumpa kipato. PICHA | FRIDAH OKACHI

Alielezea Taifa Jumapili kuwa kwa miaka mitatu alikuwa ameweka Sh60,000 ambazo zilitokana na malipo yake kwenye ukusanyaji taka.

Mwangi alichukua hatua ya kuelezea kundi kiasi cha fedha alichokuwa nacho na kuwa, siku mbili baada ya kujieleza kwake, akaona matunda, kundi hilo lilipomsaidia na Sh250,000 ambazo zilimzawadi Tuktuk aliyokuwa akinuia kununua.

Patrick Mutsia kutoka Uthiru anafurahia jinsi maisha yalivyo baada ya kuacha uhalifu.

Bw Mutsia alichukua miezi sita baada ya kuacha matumizi ya dawa za kulevya na pombe kupindukia.

Katika kituo cha polisi cha Mutuini, rekodi zilionyesha kuwa amewahi kuwa mhalifu.  Hali yake ilianza kubadilika baada ya miaka miwili, akawa mwenye rekodi safi na hadi akafanya kozi ya udereva.

Yvonne Wamalwa, mkewe Patrick anasema miaka miwili baada ya mumewe kujiunga na kundi hilo, alibadilika na sasa anatekeleza majukumu ya nyumbani ipasavyo.

Katika mtaa wa Muthua, Richard Mutsia anafurahia kazi yake ya mkono. Akiwa muuzaji na fundi wa viatu, Team Kifagio ilimpa Sh50,000 kutokana na kukosa kazi ya ofisi.

“Wakati ulifika nikasema hata mimi nataka kuwa mchafu kwa njia nzuri. Nilisanya taka nikiwa na tumaini la kufanya kazi yangu ya biashara. Sasa hivi ona nina duka,” alinena akiwa na tabasamu.

Martin Mwaniki ambaye ni kiongozi wa kundi la Kifagio, anasema kuwa baadhi ya vijana wengi katika mitaa hujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya kutokana na ukosefu wa ajira.

“Wakati mwingine vijana huchanganyikiwa  kutokana na matatizo ya hapa na pale. Vijana ninao ambao wanatumia mihadarati lakini siwezi kufanikisha ndoto zao iwapo hawana nia ya kubadilika kibinafsi kwa kupunguza pombe, utumiaji wa dawa za kulevya na uhalifu,” alisema Bw Mwaniki.

 Bw Mwaniki anaongezea kuwa kundi lake hukusanya taka katika nyumba zaidi ya 300 ambazo malipo yake hutofautiana kutokana na maelewano kati ya kundi hilo na wenye nyumba.

Malipo yao yakiwa ni kati ya Sh200, Sh150, au Sh100 kwa kila nyumba kila mwezi.

  • Tags

You can share this post!

Pasta amuumbua mkewe hadharani, waumini wabaki na alama ya...

Waliopigia Azimio wasahau nyadhifa za kuteuliwa, wasubiri...

T L