• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Vya bwerere ndivyo tegemeo la vigogo

Vya bwerere ndivyo tegemeo la vigogo

NA BENSON MATHEKA

MTINDO wa wanasiasa kuacha azma zao za kugombea viti mbalimbali ili kutegea nyadhifa katika serikali kuu iwapo mirengo wanayounga mkono itashinda na kuunda serikali umeanza kushuhudiwa nchini.

Wadadisi wanasema sababu ya wanasiasa hao kuamua kutotetea viti vyao ni kukosa umaarufu mashinani, kuogopa kutumia rasilimali zao kisha wakose kushinda viti na kushawishiwa na viongozi wa vyama au miungano ya kisiasa wanayounga mkono wanaowaahidi nyadhifa serikalini wakishinda.

Wiki hii, Gavana wa Kitui, Bi Charity Ngilu alikuwa wa hivi punde kuamua kutotetea kiti chake baada ya kuahidiwa wadhifa katika serikali ya kitaifa iwapo muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya utashinda uchaguzi wa Agosti 9 na kuunda serikali.

Mgombea urais wa muungano huo, Bw Raila Odinga alisema ingawa Bi Ngilu alikuwa ameidhinishwa na Tume ya Uchaguzi (IEBC) kutetea kiti hicho, hatashindana na wapinzani wengine kwa wadhifa huo katika Kaunti ya Kitui bali atakuwa naye katika serikali ya kitaifa.

Duru zasema Bi Ngilu hakunuia kutetea kiti kutokana na ushindani mkali kutoka kwa wapinzani.

Gavana huyo anasema ameamua kuwa mlezi wa viongozi wanawake wanaochipuka, jukumu atakalotimiza vyema akiwa katika serikali ya kitaifa.

Ingawa wanasiasa wanaoacha azma zao za kutetea viti tofauti wakitegea kuteuliwa katika serikali kuu wameongezeka, wachanganuzi wanasema huenda mipango yao ikagonga mwamba ilivyofanyikia kwa Seneta wa Kaunti ya Tharaka Nithi, Prof Kithure Kindiki.

Wakili huyo alijiondoa katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Tharaka Nithi baada ya kuahidiwa wadhifa wa mgombea mwenza wa Naibu Rais William Ruto wa chama cha UDA uliomwendea mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua.

“Japo kuna sababu kadhaa za wanasiasa kuacha azma zao ili kuzawidiwa na vigogo wanaowaunga mkono, kuna hatari ya kuambulia patupu. Hata hivyo, hatari hii haiwezi kulinganishwa na kutumia mamilioni kwenye kampeni na kuambulia patupu mtu akijua sio maarufu kwa wapigakura,” asema mdadisi wa siasa Isaac Gichuki.

Wengine waliojiondoa kwenye uchaguzi mkuu ujao ni kiongozi wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi ambaye alitupilia mbali nia ya kuwania urais na kumuunga Dkt Ruto akimezea mate wadhifa mkubwa iwapo Naibu Rais atashinda uchaguzi.

Bw Mudavadi ni kati ya vinara wa muungano wa Kenya Kwanza unaojumuisha vyama vya ANC, UDA na Ford Kenya na kuungwa mkono na vingine 10.

Tofauti na vinara wenzake katika muungano huo, Bw Mudavadi hagombei kiti chochote.

Hali sawa na hiyo inamkabili kiongozi wa chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka aliyetupilia mbali ndoto yake ya kugombea urais na kumuunga Bw Odinga aliyemuahidi wadhifa wa Mkuu wa Mawaziri iwapo Azimio itashinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Wadhifa ambao Bw Musyoka na Bw Mudavadi wameahidiwa hauko katika katiba.Wengine wanaosubiri kudandia katika nyadhifa muhimu katika serikali ijayo ni mbunge wa Mumias Mashariki, Benjamin Washiali (UDA/ Kenya Kwanza) ambaye hatetei kiti chake, Seneta wa Baringo Gideon Moi ( Kanu/Azimio), Sabina Chege (Jubilee/ Azimio), Peter Munya (PNU/Azimio), Ukur Yatani (Upya/Azimio) na aliyekuwa mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth.

Bw Moi aliteuliwa na chama chake kugombea urais lakini akamuunga Bw Odinga baada ya chama chake kuwa miongoni mwa 26 vilivyotia saini mkataba wa Azimio.

Bw Munya aliacha azma yake ya kugombea ugavana wa Meru na ameahidiwa wadhifa wa Waziri wa Kilimo katika serikali ya Azimio.

Bi Chege alitangaza kutotetea kiti cha Mwakilishi wa Kike wa Murang’a naye Bw Yatani alitupilia mbali azma ya kugombea ugavana wa Marsabit.

Bw Kenneth hagombei wadhifa wowote na inasemekana anamezea mate uwaziri katika serikali ya Azimio baada ya kuwekeza rasilmali zake katika kampeni za Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

PENZI LA KIJANJA: Ni sharti upige muhuri ndoa yako!

Majaji wasema sheria ya kuchelewesha talaka haina mashiko

T L