• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Wanasiasa wakerwa na matamshi ya Junet Mohamed

Wanasiasa wakerwa na matamshi ya Junet Mohamed

NA WANGU KANURI

Matamshi ya mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed yakimsuta seneta Isaac Mwaura yaliibua gumzo katika mitandao ya kijamii huku watu wanaoishi na ulemavu nchini Kenya wakishutumu vikali maneno yake.

Junet alikuwa akimwandama Raila Odinga Kaunti ya Turkana katika pilkpilka za kuwarai Wakenya wanaoishi huko kupigia debe mchakato wa BBI aliposema kuwa seneta Isaac Mwaura aliikoboa rangi ya ngozi yake ili aweze kuteuliwa kwenye bunge.

Ubaguzi huu wa kirangi uliwafanya wanasiasa wengi wengine kumkosoa mbunge huyo.

“Junet Mohammed na ODM wanaonekana kuwa na maoni finyu kuhusu watu walio na ulemavu nchini humu. Kumsuta Isaac Mwaura si haki, hakukufaa na anapaswa kujutia matamshi hayo. Itakuwa haki endapo Junet atapambana na mkono wa sheria kwa tabia yake potovu,” akaandika @MilicentOmanga.

“Hii katu haipaswi. Ni ukiukaji wa haki za kimsingi za Mwaura na haipaswi kuvumiliwa. Junet Mohammed sharti aletwe mbele ya haki!!” akasema @MigunaMiguna.

“Huyu ni Junet Mohamed, crème de la crème wa ODM, kiongozi wa sasa wa serikali ya handsheki na kiongozi wa ngazi ya juu bungeni, msaidizi wa mwenyekiti wa sekretarieti ya BBI ambaye mada yake ni ‘kuitoa nchi ya mahusiano ya kidamu na kuifanya nchi yenye maadili.’ Kwa ufupi anasema kuwa albino si watu halisi wanakoboa rangi yao. Yasikitisha,” akaandika @kipmurkomen.

Jumapili asubuhi, mheshimiwa Junet aliomba msamaha kwa watu wanaoishi na ugonjwa wa ualbino kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter.

“Ningependa kuomba msamaha kwa watu waliozaliwa na ugonjwa wa ualbino. Maneno yangu hayadhihirishi kamwe maoni yangu kwao kama raia wan chi hii. Maneno yangu yalikuwa yakilenga tabia iliyooza ya Isaac Mwaura ambaye anatumia vibaya ulemau wake ili kujinufaisha mwenyewe na kuchochea vita,” akaandika @JunetMohamed.

Matamshi yake Junet yaliwafanya wakuu nchini kutoka tume ya watu wanaoishi na ulemavu kutaka Junet achukuliwe hatua za kisheria na pia kuomba msamaha kwa Isaac Mwaura na jamii ya watu wanaoishi na ualbino nchini. Isitoshe waliwarai wanasiasa kuzingatia wanayosema na katu wasichanganye ulemavu na uanasiasa kwani huko ni kuwavunjia heshima na haipaswi kuwa hivyo. Walitamatisha kwa kusema kuwa viongozi wanapaswa kuwa vielelezo vyema kwenye jamii.

Wakenya hali kadhalika walikuwa kwenye kinyanganyiro cha vuta nikuvute huku wengine wakidai kuwa Isaac Mwaura alipaswa kushutumiwa na wengine wakiyapinga maoni hayo.

“Unaweza mtusi Isaac Mwaura lakini si ulemavu wake. Tunao watoto wenye ulemavu uo huo shuleni. Unafikiri watajihisi vipi? Watoto hao wengine keshoye watawaambia watoto wenye ulemavu wa ualbino kuwa wameikoboa rangi yao,” akaandika @IkeOjuok.

“Kila mtu anayemtetea Junet Mohamed ni mmoja wa shida tuliyonayo. Matamshi yake kwa Isaac Mwaura ni ya kuvunja heshima na yenye kubagua na sharti yashutumiwe,” akatamatisha @BravinYuri.

“Ili Mwaura aheshimiwe kama kiongozi wa watu wenye ulemavu, lazima ajiheshimu. Yeye huwatumia watu wanaoishi na ulemavu ili kufika bungeni kisha kuanza kuangazia tumbo yake. Je kuna bili yoyote iliyodhaminiwa na yeye?,” akaandika @mwalimu_dida.

“Isaac Mwaura ni gaidi wa kisiasa na tapeli. Junet alifanya vyema kucheza kadi ya ulemavu kwake. Aliwarai vijana wa Githurai kumpiga na mawe baba. Simwonei huruma Mwaura,” akatamatisha @DonaldBKipkorir.

You can share this post!

CHOCHEO: Hadaa ya mapenzi huja na kilio

Kambi ya Olunga imani tele ikiendea Ulsan Hyundai