• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Wandani wa Raila wakataa wito wa Mudavadi waunge serikali

Wandani wa Raila wakataa wito wa Mudavadi waunge serikali

NA DERICK LUVEGA

WITO wa Mkuu wa Mawaziri, Bw Musalia Mudavadi, kutaka wanasiasa wa upinzani eneo la Magharibi wajitenge na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, na kuunga mkono serikali ya Rais William Ruto umeibua hisia mseto miongoni mwa wanasiasa.

Baadhi ya wafuasi wa Bw Odinga eneo hilo wakiongozwa na Seneta wa Vihiga, Bw Godfrey Osotsi, wamepuuzilia mbali wito wa Bw Mudavadi.

Mnamo Jumatatu katika maadhimisho ya 43 ya tamasha la kitamaduni la jamii ya Wamaragoli, Bw Mudavadi aliomba wanasiasa walio wafuasi wa Bw Odinga kumuunga mkono Rais Ruto ili eneo hilo linufaike na serikali iliyopo mamlakani.

Bw Mudavadi alirai wanasiasa wa muungano wa upinzani Azimio la Umoja- One Kenya katika eneo la Magharibi, kukumbatia utawala wa serikali ya Rais Ruto.

Isitoshe, aliongeza kuwa tayari muungano tawala wa Kenya Kwanza umempokea Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Cotu), Bw Francis Atwoli.

Lakini jana Alhamisi Bw Osotsi aliapa kuongoza viongozi wenzake wa jamii ya Mulembe — yenye idadi kubwa ya wapiga kura — kuendelea kumuunga Bw Odinga na muungano wa Azimio.

Hata hivyo, kuna baadhi ya wanasiasa wamepokea vyema wito wa Bw Mudavadi akiwemo Mbunge wa Kimilili, Bw Didmus Barasa, na mwenzake wa Emuhaya, Bw Omboko Milemba.

Wabunge hao walisema eneo la Magharibi limo serikalini kufuatia hatua ya Bw Mudavadi na Spika wa Bunge la Kitaifa Bw Moses Wetang’ula kujiunga na Kenya Kwanza kuelekea uchaguzi mkuu.

Huku Bw Osotsi akishutumu serikali ya Dkt Ruto kwamba haijatekeleza ahadi ilizotoa kwa Wakenya wakati wa kampeni, Bw Milemba aliomba muda ili eneo hilo lianze kuvuna ahadi hizo.

Katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, eneo la Magharibi lilipigia kura madiwani, wabunge na magavana wengi kutoka mrengo wa Bw Odinga.

Akipuuzilia mbali wito wa viongozi wa jamii ya Mulembe waungane na serikali ya Kenya Kwanza, Bw Osotsi alisisitiza kuwa wao walipigiwa kura kuhudumu katika upinzani.

Alisisitiza kwamba wataendelea kuwa waaminifu kwa Bw Odinga na kuikosoa serikali.

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto aongoza taifa kumwomboleza mtangazaji Kasavuli

Wanabunduki kwenye mizani ya Brighton leo Jumamosi

T L