• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Wanyonyi anyimwa tikiti kuwania ugavana Nairobi

Wanyonyi anyimwa tikiti kuwania ugavana Nairobi

NA WINNIE ONYANDO

MBUNGE wa Weslands, Tim Wanyonyi amepangwa na muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya baada ya azma yake ya kuwania kiti cha ugavana kuzimwa na tikiti kukabidhiwa aliyekuwa Naibu gavana wa Nairobi, Polycarp Igathe.

Bw Wanyonyi ambaye amekuwa Mbunge wa Westlands kwa miaka 10 sasa atalazimika kurudi katika eneo bunge la Westlands ili kutetea kiti hicho.

Haya yanajiri kufuatia tangazo lililotolewa jana na Kinara wa ODM, Raila Odinga ambaye alisema Bw Wanyonyi atawania kiti cha ubunge Westlands.

Mbunge huyo ambaye alianza kampeni zake za kuwania kiti cha ugavana Nairobi miaka miwili iliyopita kufikia jana hakuwa amezungumzia wala kutoa msimamo wake kuhusu maamuzi ya muungano huo yaliyotolewa na Bw Odinga.

Bw Wanyonyi amekuwa akijipigia debe kila eneo jijini Nairobi huku akiuza sera zake kwa wananchi.

Japo mazungumzo ya maelewano yalikuwa yakiendelea Ikuluni kuhusiana na kiti hicho, Bw Wanyonyi naye amekuwa akiwahakikishia wafuasi wake kuwa bado atawania kiti hicho na hata kundelea kuwauzia sera zake.

Kwa upande wake, Bw Odinga alisema kuwa safari ya Nairobi imeng’oa nanga na kuwa walioteuliwa sasa hawana budi kunadi sera zao kwa wananchi.

Mgombea mwenza wa Bw Igathe ni Philip Kaloki, Edwini Sifuna amepewa tikiti ya kuwania kiti cha useneta huku Esther Passaris atawania kiti cha mbunge mwakilishi wa kike kupitia tikiti ya muungano huo.

“Namshukuru mfanyabiashara Richard Ngatia na Bw Wanyonyi kwa kuamua na kuwaachia wenzao nafasi. Safari ya Nairobi imeanza rasmi,” akasema Bw Odinga.

Kwa upande mwingine, Bw Ngatia ameteuliwa kuwa Balozi Maalum wa Biashara nchini.

“Kutoka hapa, Bw Ngatia ndiye balozi maalum wa biashara nchini. Namshukuru sana kwa kuwa japo amekuwa akiendeleza kampeni zake, aliamua kumwachia Bw Igathe,” akasema Bw Odinga.

Hata hivyo, tangazo hilo la Bw Odinga huenda likaleta utata katika eneo bunge la Westlands.

Hii ni kwa sababu wakati uo huo wa tangazo, kura za mchujo wa chama cha ODM zilikuwa zikiendelea huku mwaniaji wa kiti hicho kupitia chama cha ODM tayari alikuwa amepiga kura yake.

Mwaniaji wa kiti hicho, Philip Kisia ambaye alikuwa karani wa Nairobi tayari alikuwa amepiga kura yake wakati ambapo Bw Odinga alikuwa akitoa tangazo hilo.

  • Tags

You can share this post!

Ukraine yalalama Urusi inaua na kuzika maelfu ya raia wake

Msako waanzishwa dhidi ya genge la vijana wanaopora wenyeji...

T L