• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:55 AM
Wapinzani wa Nassir walia serikali ya Joho inawatesa

Wapinzani wa Nassir walia serikali ya Joho inawatesa

NA WAANDISHI WETU

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa, imezidi kulaumiwa kwa madai ya kuwahangaisha wawaniaji wa ugavana wanaounga mkono mrengo usiokuwa wa Gavana Hassan Joho.

Aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar, ambaye anawania ugavana Mombasa kupitia chama cha UDA, amedai kuwa Bw Joho anahangaisha kampeni zake kwa kumnyima nafasi ya kuweka mabango yake mjini na mitaani.

Malalamishi hayo yametokea siku chache baada ya Naibu Gavana, Dkt William Kingi, anayewania kiti hicho kupitia chama cha PAA, kudai kuwa maafisa wa kaunti hiyo walimpokonya gari lake rasmi la kazi.

Tofauti na wanasiasa wengine wengi ambao wamekuwa wakiweka mabango yao kwa muda sasa, mabango ya Bw Omar hayajaonekana.

Kulingana na Bw Omar, amekuwa akitaka kutundika mabango yake lakini amenyimwa nafasi, huku akimlaumu Bw Joho kwa masaibu hayo .

“Wameambia hao watu wasitupe nafasi kuweka mabango yetu ili waweke yao. Mimi sitababaishwa na mwanasiasa yeyote,” akasema Bw Omar anayewania ugavana kwa mara ya pili baada ya kubwagwa na Gavana Joho katika mwaka wa 2017.

Katika uchaguzi ujao wa Agosti, chama cha ODM kimemsimamisha Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, kuwania urithi wa kiti hicho akiungwa mkono na Bw Joho.

Hata hivyo, Katibu wa Kaunti ya Mombasa, Bw Joab Tumbo, alipinga madai ya Bw Omar akisema serikali ya kaunti hiyo haihusiki katika mambo ya kuidhinisha mabango.

“Mabango huwekwa na kampuni za kibinafsi, kazi yetu ni kuchukua kodi za mauzo. Kama anaanza kubabaika kwa sababu ya uchaguzi mkuu, apambane na hali yake,” akasema Bw Tumbo.

Wiki iliyopita, Dkt William Kingi, aliibua malalamishi akidai kuwa maafisa wa kaunti walimpokonya gari lake rasmi la kikazi.

Dkt Kingi alilalamika kuwa gari hilo lilichukuliwa kutoka nyumbani kwake bila yeye kuarifiwa ilhali bado ana majukumu ya kutekeleza kama naibu gavana.

Mbali na wawili hao, wawaniaji wengine wa ugavana wa Mombasa ni aliyekuwa mbunge wa Nyali, Bw Hezron Awiti wa chama cha Vibrant Democratic Party, Bw Daniel Kitsao aliye mwaniaji huru, Said Abdalla (Usawa Kwa Wote), na Shafii Makazi (UPIA).

Awali, Bw Awiti alikuwa amedai kuna njama ya kumpokonya sehemu ya ardhi ambapo amejenga kivutio cha utalii cha Mamba Village, ingawa hakutaja wahusika halisi.

Hatima ya aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, kuwania kiti hicho bado haijajulikana kwani pingamizi dhidi yake kutoka kwa Tume ya Uchaguzi (IEBC), zingali kortini.

Mashirika yalipinga azma yake hiyo mahakamani kwa vile alibanduliwa Nairobi kwa makosa ya kimaadili.

Katika kampeni zake, Bw Omar na wanachama wengine wa UDA hudai kuwa utawala wa ODM Mombasa haujaleta mafanikio kwa wakazi.

Mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali alimpigia debe Bw Omar akisema ana tajriba ya kutetea wananchi ili watendewe haki.

“Omar aliyekuwa kamishna katika tume ya kutetea haki za binadamu, alikuwa kiongozi wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Moi hadi akafukuzwa na utawala wa (aliyekuwa rais Daniel) Moi, amekuwa seneta wa Mombasa ambaye alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha mikakati inaendelea vyema inavyotakikana,” Bw Ali alisema.

  • Tags

You can share this post!

Damaris Nyiva ‘Minam’: Mwalimu na mwigizaji...

KWPL: Kangemi, Kayole na Bunyore zaangukiwa na shoka

T L