• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Wetang’ula apuuza Eseli mzozo ukitokota Ford- Kenya

Wetang’ula apuuza Eseli mzozo ukitokota Ford- Kenya

Na BRIAN OJAMAA

MZOZO wa uongozi ndani ya chama cha Ford- Kenya bado haujazimwa baada ya kiongozi wa chama hicho, Bw Moses Wetang’ula kupuuzilia mbali hatua ya waasi wa chama hicho kuitisha kongomano la wajumbe (NDC).

Kwenye tangazo la kulipiwa lililochapishwa katika gazeti la Saturday Nation, Mbunge wa Tongaren, Bw Eseli Simiyu alisema kongamano hilo litafanyika mnamo Novemba 6, mwaka huu.

Lakini akihutubia wanahabari nyumbani kwake Kanduyi, Kaunti ya Bungoma jana, Bw Wetang’ula alisema Dkt Eseli hana mamlaka ya kuendesha shughuli zozote kwa niaba ya chama hicho.

“Tumeona tena kwamba Eseli na kundi lake wanaendesha vitendo haramu vinavyokiuka katiba ya chama. Hatutavumilia vitendo kama hivyo,” akasema Bw Wetang’ula.

Bw Wetang’ula ambaye ni Seneta wa Bungoma alisema chama cha Ford Kenya kinazingatia sheria, taratibu, demokrasia na kinaheshimu maagizo ya mahakama na utawala wa kisheria.

Alisema Dkt Eseli alisimamishwa kama Katibu Mkuu baada ya kuongoza mapinduzi ya uongozi katika mkahawa wa Radisson Blue, Nairobi mwaka jana.

Hata hivyo, mapinduzi hayo yalitibuka baada ya upande wa Wetangula kuelekea mahamakani kutafuta suluhu.Bw Wetang’ula alisema kusimamishwa kwa Eseli kulithibitishwa na Mahakama Kuu na hivyo hana idhini ya kuendesha shughuli zozote kwa niaba ya Ford Kenya.

Bw Wetang’ula alisema Katibu Mkuu wa Ford Kenya, ni Millicent Abudho.“Ningependa kuwaambia wanachama wetu wapuuze tangazo la kutoka kwa Eseli kuhusu NDC kwani hana mamlaka ya kuitisha mkutano huo,” akasema.

You can share this post!

Kaunti za Pwani kusaka ?watalii kama eneo moja

Wafalme wa kuhadaa vijana