• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:50 AM
Wiper yajitenga na Gideon Moi kuhusu kuunga Raila 2022

Wiper yajitenga na Gideon Moi kuhusu kuunga Raila 2022

Na PIUS MAUNDU

CHAMA cha Wiper, kimetofautiana na Kanu kuhusu ushirikiano wa Muungano wa One Kenya Alliance (OKA) na chama cha ODM kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Mwenyekiti wa Kanu, Bw Gideon Moi, Ijumaa alisema kuwa OKA haikuwa na tofauti na Bw Odinga kwa kuwa wana lengo moja kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Hata hivyo, viongozi wa chama cha Wiper, kinachoongozwa na aliyekuwa makamu rais, Bw Kalonzo Musyoka, walijitenga na kauli ya Bw Moi.

“Lazima OKA itakuwa na mgombea urais kumenyana na Raila (kiongozi wa ODM) na Naibu Rais William Ruto kwa kuwa mashindano kati ya Raila na Ruto yanaweza kuzua ghasia Kenya. Tunahitaji uongozi mbadala na lazima utatoka OKA,” alisema Seneta wa Kaunti ya Makueni aliye naibu mwenyekiti wa Wiper, Bw Mutula Kilonzo Junior.

Seneta huyo alimshutumu Bw Odinga kwa usaliti hasa kwa kukosa kumuunga mkono kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka jinsi walivyokubaliana mwaka wa 2017 chini ya muungano wa National Super Alliance (NASA).

Alipinga madai kuwa Bw Musyoka anashirikiana na Bw Odinga na anaunga mkono azma yake ya kuwania urais.

“Tulitarajia Bw Odinga angeidhinisha azma ya Bw Musyoka ya urais kwa mujibu wa mkataba wa 2017 ulioshuhudiwa na Profesa Makau Mutua na Profesa Kivutha Kibwana, wote ambao walihudhuria kongamano la Azimio la Umoja. Tumekata tamaa na tutabuni njia zetu za kufanya kampeni. Lakini hatutasahau kwamba tuliwasaidia na wakati ulipofika wa kutusaidia walikataa. Tutatafuta uongozi,” akasema.

Alisema kuwa muungano huo uko tayari kutafuta uongozi na hata kutoa tahadhari kwa Dkt Ruto na Bw Odinga kujitayarisha kwani wana imani kuwa wataibuka washindi.

Kadhalika, alikashifu hatua ya mabwanyenye wanaotoka eneo la Mlima Kenya kwa kumuunga mkono kinara huyo wa ODM kuwania urais.

Alisema kuwa viongozi wa Mlima Kenya walijua vizuri kuwa wangemwidhinisha Bw Odinga huku wakiwadanganya viongozi wa OKA na hata kuahidi kuwa wangewaunga mkono.

Seneta huyo alisema hayo kufuatia uvumi kwamba OKA ilikuwa ikitafakari kushirikiana na ODM.

“Hatuko tayari kumuunga mkono Bw Odinga,” akasema.

Vinara wa OKA Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (Amani National Congress), na Moses Wetangula (Ford Kenya), walijitenga na Bw Odinga kwenye kongamano la Azimio la Umoja mnamo Ijumaa.

Ni Bw Moi pekee aliyehudhuria hafla ya Bw Odinga na kuashiria kuwa OKA ingeungana na Bw Odinga.

“Majeshi yetu ni moja. Raila anapopata nguvu sisi tunapata nguvu, tunapopata nguvu, Raila anapata nguvu pia,” Bw Moi alisema.

Matamshi ya Bw Moi yalichukuliwa na baadhi ya watu kuwa muungano wa OKA ulikuwa tayari kumuunga mkono Bw Odinga, jambo ambalo Bw Kilonzo alipinga vikali.

Alisema kuwa OKA iko tayari kupigana vikali kuzuia ODM kuwapokonya Bw Moi ili OKA ihifadhi sifa yake kama muungano wa kitaifa.

You can share this post!

Hisia mseto zatolewa kufuatia kauli ya Ngilu...

Uhuru asisitiza umuhimu wa umoja

T L