• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 5:29 PM
Ruto awataka viongozi wa kidini watoe mwelekeo wa kisiasa kwa waumini

Ruto awataka viongozi wa kidini watoe mwelekeo wa kisiasa kwa waumini

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amewataka viongozi wa kidini wawe mstari wa mbele kuwahamasisha wananchi washiriki katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Akiongea Jumamosi akiendesha kampeni zake za urais katika Kaunti ya Kitui, Dkt Ruto amewataka viongozi wa kidini kutumia ushawishi wao katika jamii kuwashauri Wakenya kuchagua viongozi wenye busara.

“Haitoshi kwa viongozi wa kidini kuombea taifa pekee. Wanafaa kushiriki katika shughuli za kisiasa kwa kuwaelekeza waumini na Wakenya kwa ujumla ili wawachague viongozi waadilifu na wenye rekodi ya maendeleo,” akaeleza akiwa mjini Kitui.

Aliandamana na viongozi wa eneo la Ukambani wakiwemo wabunge Victor Munyaka (Machakos Mjini), Nimrod Mbai (Kitui Mashariki), mwenyekiti wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Johnston Muthama na aliyekuwa Naibu Gavana wa Nairobi Jonathan Mueke.

Kwa upande wake Bw Mbai alisema ni vugumu kutenganisha Kanisa na siasa.

“Hii ndio maana ninatoa wito kwa viongozi wa kisiasa kutoa mwelekeo wa kisiasa kwa waumini kwa kuwataka wawahimize wawachague viongozi wenye sera za kuleta maendeleo wala sio wale wenye maneno matupu,” akasema.

Bw Mbai aliwataka viongozi wa kidini kutokubali kutishwa kwa kutangaza misimamo yao ya kisiasa.

Naye Bw Munyaka alitaka Kanisa kuendelea kuwaombea wanasiasa ili waendeshe kampeni zao kwa amani.

Kwa upande wake Bw Muthama alitoa wito kwa wakazi wa Ukambani wasikubali kuhadaiwa bali wamuunge mkono Dkt Ruto kwa sababu “yeye ndiye anayeuza sera za kuinua maisha ya watu wa tabaka la chini.”

You can share this post!

Southampton wachapa Aston Villa ligini na kuweka kocha...

TAHARIRI: Wanasiasa waache kuhadaa kwa spoti

T L