• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:04 PM
Kalonzo Musyoka amesota

Kalonzo Musyoka amesota

NA CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Kitui Mashariki Nimrod Mbai, ambaye ni mwandani wa Rais William Ruto sasa anadai kuwa kiongozi wa Wiper hana fedha za kumwezesha kufadhili kampeni za urais 2027.

Bw Kalonzo Musyoka ndiye kinara wa chama cha Wiper.

Kupitia video iliyochapishwa “Kenya Digital News”, mbunge huyo anaskika akisema Bw Musyoka hawezi kumudu kampeni ya urais kwa zaidi ya wiki moja kabla ya kufilisika.

“Endapo ndugu yetu Kalonzo ataamua kuwania urais kivyake 2027 ataendesha kampeni kwa wiki moja tu kisha atafilisika kwa sababu hana nguvu kifedha kama washindani wake wengine kama Rais Ruto na Raila Odinga,” Bw Mbai anasema huku akionekana kuwahutubia wanahabari nyumbani kwake Kitui Mashariki.

Kwa hivyo, Mbunge huyo wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) amemtaka Bw Musyoka kuweka kando ndoto yake ya urais na kubuni muungano na Dkt Ruto.

“Hawezi kushinda urais pekee yake…Kiti hicho kitahitaji mtu ambaye anaweza kutumia pesa nyingi kama Rais Ruto. Akijaribu kuzunguka Kenya mfululizo kwa wiki moja alivyofanya Ruto, atafilisika na kujiondoa,” Mbai akasema.

Mbunge huyo alimshauri Bw Musyoka kuondoa imani kuwa anaweza kuungwa mkono azma yake ya urais 2027.

“Raila amejenga himaya yake ya kisiasa kwa muda mrefu na hawezi kumpokeza Kalonzo. Kwa hivyo, Kalonzo asitarajie kuwa Raila atampisha, kwani kiongozi huyo wa ODM bado atajitosa uwanjani 2027 na bado anaonekana mwenye nguvu,” Bw Mbai anaeleza.

Mbunge huyo amemhimiza kiongozi huyo wa Wiper kuhakikisha kuwa anaungana na Rais Ruto ili jamii wa Wakamba ichume matunda ya kuwa serikalini.

“Viongozi kama Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula waling’amua mapema umuhimu wa kubuni muungamo kabla ya uchaguzi uliopita, 2022. Na wakachukua hatua hiyo kwa kujiunga na timu iliyoshinda ya Rais Ruto. Sasa Mudavadi ndiye kiongozi wa tatu kwa hadhi katika serikali kuu, ilhali Bw Wetang’ula ndiye mkuu wa asasi ya bunge, vyeo ambavyo vimechochea maendeleo katika maeneo wanakotoka,” Bw Mbai anaeleza.

  • Tags

You can share this post!

Mayatima wa Jubilee wanavyojifufua kisiasa

EACC yatakiwa kuchunguza mradi wa barabara

T L