• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Uchungu wa kuona pesa za elimu ng’ambo zikizama

Uchungu wa kuona pesa za elimu ng’ambo zikizama

NA FRED KIBOR

MPANGO tata wa kuwapeleka wamafunzi kutoka Kaunti ya Uasin Gishu kuenda ughaibuni kusomea katika vyuo vikuu vya Laurea, Jyvaskylla, na Tampere unachunguzwa, huku wazazi wakiandamana kushinikiza warejeshewe pesa walizotoa kuufanikisha.

Kaunti ya Uasin Gishu wakati wa utawala wa Jackson Mandago ambaye sasa ni Seneta wa kaunti hiyo, iliingia kwa mkataba huo ili wanafunzi waende nchini Finland.

Wakiwa huko, wanafunzi walikabiliwa na msongo wa mawazo ilipobainika karo haikuwa imelipwa jinsi ilivyokuwa kwenye mkataba.

Hata mwanafunzi mmoja alijitia kitanzi mnamo Mei 2023 akiwa katika taifa hilo la ughaibuni.

Kwa baadhi ya wanafunzi, japo walilipa hela kwa mfuko uliokuwa chini ya uangalizi wa serikali ya kaunti, hawajawahi kuondoka nchini.

Mzee John Tirop, ameambia Taifa Leo aliuza kipande cha ardhi nusu ekari kupata Sh1.2 milioni za kumwezesha binti yake kuenda ng’ambo kupata elimu.

“Tayari aliyenununua kipande hucho cha ardhi amejenga nyumba anaishi lakini kinaya ni kwamba binti yangu yungali hapa nyumbani. Ninataka kaunti inirudishie hela nimtafutie mwanangu fursa za elimu kwingineko,” amesema Mzee Tirop.

Nao wazazi wa Brian Kimutai walilipa Sh1.2 milioni asomee shahada ya digrii katika Chuo Kikuu cha Tampere nchini Finland lakini mwaka mmoja umepita akiwa angali nyumbani.

Kijana huyo anataka warejeshewe pesa hizo.

“Kila wakati hata usingizini tunalia kwa kufanyiwa utapeli mchana peupe,” akasema kijana Kimutai.

Masaibu ya Kimutai ni kama ya Benjamin Cheboson, mbaye wazazi wake waliuza mali chungu nzima kupata Sh1.2 milioni, lakini fursa ya kuenda kujiunga na Chuo Kikuu cha Laurea kusomea utabibu haijawahi kuwadia.

Kwa sasa anafanya kazi katika kilabu kujaza kibaba cha kidogo ambacho wazazi wake wanapata ili kukidhi mahitaji ya nyumbani.

“Tunataka waturejeshee pesa kwa sababu ni wazi kwamba hakuna kuenda nchini Finland,” akasema Bw Cheboson.

Mtetezi wa haki za binadamu Kimutai Kirui anataka Gavana wa sasa wa Uasin Gishu Jonathan Bii na naibu wake, ambao walirithi ‘sakata’ hiyo, wajiuzulu kwa sababu hawajamakinikia suala hilo.

“Ikiwa kweli wawili hao hawakuhusika kwa sakata hiyo, basi hawangekuwa wanatetea walioanzisha mpango huo wa kupora hela kutoka kwa wazazi wenye ari na bidii ya kuwasomesha watoto wao,” akasema Bw Kirui.

Naye mwaniaji ugavana Bundotich Zedekiah Kiprop almaarufu ‘Buzeki’ ameandika katika mitandao ya kijamii akisema anahisi ni vyema Gavana Bii almaarufu ‘Koti Moja’ awajibikie suala hilo.

Aidha, Buzeki anataka wananchi waliolaghaiwa kuendelea kuandamana hadi wapate haki.

  • Tags

You can share this post!

Omanyala na wenzake mawindoni kutafuta tiketi ya riadha za...

‘Padri na mrembo wake walijienjoi kwa zaidi ya miaka...

T L