• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 7:55 PM
CECIL ODONGO: Mali ya umma isitumiwe kufadhili afisi zisizotambulika rasmi kikatiba

CECIL ODONGO: Mali ya umma isitumiwe kufadhili afisi zisizotambulika rasmi kikatiba

NA CECIL ODONGO

AFISI za wake wa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi, zifutiliwe mbali.

Wiki jana, Bw Mudavadi alifungua afisi ya mkewe, Bi Tessie Mudavadi, ambayo alisema itaoanisha majukumu yake na yale ya afisi za Naibu Rais na Rais.

Mwanzo, kulingana na utamaduni ambao umekwepo tangu Kenya ijinyakulie huru, kumekuwa na afisi ya mke wa Rais maarufu kama Mama wa Taifa.

Wakati wa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta, mkewe Margaret alikuwa na afisi ambayo ilijikita katika masuala ya haki za wanawake na vita dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Bi Margaret Kenyatta atakumbukwa sana kwa kuanzisha miradi kadhaa ikiwemo ule wa Beyond Zero ambao ulishughulikia afya ya watoto, akina mama na kwa ujumla kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.

Wakati wa utawala wa Mwai Kibaki, mkewe Mama Lucy Kibaki ndiye alitambuliwa kuhusika katika shughuli za kitaifa. Wala haikuwa mke wa Moody Awori (kipindi cha kwanza) au Kalonzo Musyoka (kipindi cha pili) waliokuwa makamu wa Rais.

Vivyo, baada ya Kenya kupata uhuru ni Mama Ngina Kenyatta ndiye alishirikiana na Mzee Jomo Kenyatta kuhusu masuala mbalimbali ya taifa.
Hata sasa mkewe Rais Ruto, Rachel, ndiye anastahili kuwa mstari wa mbele kuhusu miradi inayohusiana na afisi yake.

Hili la wake wa Gachagua na Mudavadi kujiundia afisi ambazo majukumu yake hayajabainika wazi kikatiba, halifai.

Iwapo afisi hizo zitaendelea kuwepo basi wawili hao wajigharamie pesa zinazohitajika kuziendesha badala ya hela za mlipaushuru.

Hatua ya wawili hao kuunda afisi za wake zao pia inafasiriwa kama ushindani kati yao ndani ya utawala wa Kenya Kwanza.

Rais William Ruto alisema serikali yake inalenga kupunguza gharama za matumizi. Je, itafaulu kivipi iwapo viongozi wenzake wanajibunia afisi ambazo hazipo kwenye Katiba?

  • Tags

You can share this post!

Faida za kula zukini

KIKOLEZO: Ifahamu hii sanaa ya ucheshi isiyo kawaida

T L