• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 10:55 AM
Maandamano yaendelee sambamba na mazungumzo – Raila

Maandamano yaendelee sambamba na mazungumzo – Raila

NA BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga, ametangaza kuwa muungano wa upinzani utarudia maandamano ya kila wiki baada mwezi Mtukufu wa Ramadhan kukamilika huku mazungumzo ya maridhiano yakiendelea bungeni.

Akisema kwamba muungano unaotawala wa Kenya Kwanza haujaonyesha nia njema ya kufanikisha mazungumzo kwa kupuuza baadhi ya matakwa ya Azimio, Bw Odinga alisema maandamano na mazungumzo yatafanyika sambamba.

“Nimewasikia. Mnataka maandamano yarudi. Punde baada ya Ramadhan, nitatangaza wakati maandamano yatarudi kote nchini. Maandamano na mazungumzo yatafanyika sambamba,” Bw Odinga alisema katika ukumbi wa Ufungamano, Nairobi baada ya kukutana na vyama vya wafanyakazi, mashirika yasiyo ya serikali, mashirika ya kijamii na viongozi wa kidini.

Bw Odinga alisema kwamba ingawa Azimio ilisitisha maandamano kufuatia ombi la Rais William Ruto aliyependekeza mazungumzo, muungano huo wa upinzani hautakubali kutumiwa kama muhuri wa kuidhinisha hatua na sera zinazoumiza Wakenya.

Baadhi ya matakwa ya Azimio ni kupunguzwa kwa gharama ya maisha, kufunguliwa kwa sava ambazo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilitumia katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, kusitishwa kwa mchakato wa kuajiri makamishna wapya wa IEBC na kurejeshwa kazini kwa makamishna wane waliokataa matokeo ya urais maarufu kama Cherera 4.

Kenya Kwanza imeshikilia kuwa suala litakalojadiliwa kwenye mazungumzo ni kuhusu mchakato wa kuajiri makamishna wapya wa IEBC.
Azimio pia inataka mazungumzo hayo yapanuliwe kuhusisha wadau wengine nje ya bunge, pendekezo ambalo Kenya Kwanza imekataa ikisema sio la kikatiba.

Jana Alhamisi, Bw Odinga alisema kwamba hakuna kinachozuia mazungumzo nje ya bunge akisema yamewahi kufanyika na kufaulu.

“Tumewahi kuwa na mazungumzo na mdahalo wa kitaifa nje ya bunge, mengine yalifanyika hata katika hoteli kama serena na hayakutajwa kuwa yasiyo ya kisheria,” alisema.

Kiongozi huyo wa upinzani alisema kwamba Azimio haitakubali kutumiwa kuidhinisha ushindi wa Rais William Ruto.

“Kenya Kwanza imekuwa ikitumiwa kama muhuri wa kila kitu na hatutakubali kutumiwa kama muhuri, hatutatishwa,” alisema.

Waziri Mkuu huyo wa zamani ameitisha mkutano wa kisiasa katika uwanja wa Kamukunji Jumapili ijayo ambao huenda akatumia kutangaza siku ya kurudia maandamano kote nchini.

Alisisitiza kuwa ni haki ya kidomkrasia ya Wakenya kuandamana na akalaumu polisi kwa kutumiwa vibaya kushambulia wafuasi wa Azimio wakifanya maandamano ya amani.

“Tumeagiza mawakili wetu na wanaendelea na kutayarisha kesi dhidi ya maafisa wa polisi waliotumia nguvu kupitia kiasi kwa waandamanaji na wanahabari wasio na hatia. Tutawashtaki katika mahakama kuu zaidi ulimwenguni,” Bw Odinga alisema.

Vinara wa Azimio Kalonzo Musyoka, Martha Karua, Eugene Wamalwa na viongozi wa mashirika ya kijamii walisema serikali haina nia njema katika mazungumzo iliyoitisha.

Mashirika ya kijamii yalisisitiza kuwa lazima suala la kupunguza gharama ya maisha lijadiliwe katika mazungumzo yatakayohusisha wadau nje ya bunge.

  • Tags

You can share this post!

 Seneta ashtakiwa kwa kukwepa kulipa ushuru

Aomba aachiliwe huru kuendeleza biashara ya dhahabu feki

T L