• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 6:55 PM
Wanafunzi South B PEFA Academy wachagua viongozi wakihimizwa kukumbatia demokrasia

Wanafunzi South B PEFA Academy wachagua viongozi wakihimizwa kukumbatia demokrasia

NA SAMMY KIMATU

WANAFUNZI katika shule ya South ‘B’ PEFA Academy iliyoko kaunti ndogo ya Makadara wamejawa na tabasamu baada ya kupata viongozi wapya  waliochaguliwa mnamo Ijumaa wiki jana.

Msimamizi wa Idara ya Serikali ya Wanafunzi Bw Brian Otim ameambia Taifa Leo kwamba uchaguzi huo uliendeshwa kuambatana na mtaala uliopo chini ya Wizara ya Elimu nchini.

“Wanafunzi wanahimizwa kuchagua viongozi wao na wakati huo huo kufundishwa kuhusu umuhimu wa demokrasia na haki zao kikatiba,” Bw Otim aliye kadhalika naibu wa mwalimu mkuu akasema.

Msimamizi wa Idara ya Serikali ya Wanafunzi Bw Brian Otim ambaye vile vile ni naibu wa mwalimu mkuu. PICHA | SAMMY KIMATU

Licha ya shule hiyo kuwa na idadi ya wanafunzi 487, walioshiriki walikuwa watoto 300 ikizingatiwa kwamba ni wanafunzi kutoka Gredi 3 kuenda juu wanaoruhusiwa kupiga kura.

Kilele cha hafla hiyo kilikuwa wakati wa uchaguzi wa Rais wa Wanafunzi ambapo wawaniaji walikuwa wanafunzi watatu.

Kulikuwa na Samuel Murithi, 13, John Thuku, 11 na Stephen Maina, 10, waliokuwa wagombeaji wa kiti hicho. Murithi na Maina ni mabinamu.

Rais wa wanafunzi shuleni South B PEFA Academy John Thuku. PICHA | SAMMY KIMATU

Kura zilipohesabiwa John Thuku aliibuka mshindi kwa kujizolea kura 140 akifuatiwa kwa karibu na Samuel Murithi aliyepigiwa kura 137 naye Maina akapata kura 20 pekee.  

Akiongea na Taifa Leo baada ya kutangazwa mshindi Thuku alisema ushindi wake umechangiwa na rafikiye wa dhati aliyeongoza kampeni za kutembea kutoka darasa moja hadi lingine kuomba kura.

“Nilikuwa na manifesto nzuri huku kampeni yangu ikiongozwa na Duncan Atambo wa Gredi 6. Ninamshukuru Mola na wanafunzi wote walionipigia kura. Nitafanya kazi kwa kujituma bila kubagua wapinzani wangu,” Thuku akaeleza.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Polisi bandia anayehangaisha wakazi Nairobi

UHC: Serikali yaambiwa ikome kuwa kupe kwa kutegemea tu...

T L