• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Gor Mahia waaga CAF Champions League baada ya kupokezwa kichapo cha jumla ya mabao 8-1 kutoka kwa CR Belouizdad ya Algeria

Gor Mahia waaga CAF Champions League baada ya kupokezwa kichapo cha jumla ya mabao 8-1 kutoka kwa CR Belouizdad ya Algeria

Na CHRIS ADUNGO

MIAMBA wa soka ya Kenya, Gor Mahia sasa watashuka kuwania taji dogo la Kombe la Mashirikisho Afrika (CAF Confederations Cup) baada ya kubanduliwa na CR Belouizdad kwenye kivumbi cha Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League).

Chini ya kocha mshikilizi Sammy ‘Pamzo’ Omollo ambaye pia anadhibiti mikoba ya Posta Rangers, Gor Mahia walidenguliwa na Belouizdad kwa jumla ya mabao 8-1 baada ya kupepetwa 2-1 katika mkondo wa pili mnamo Januari 6 ugani Nyayo, Nairobi.

Gor Mahia walijibwaga ugani kwa minajili ya mechi hiyo wakiwa na ulazima wa kusajili ushindi wa 7-0 baada ya kudhalilishwa 6-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliosakatiwa jijini Algiers, Algeria mnamo Disemba 26, 2020.

Mnamo Jumatano, Gor Mahia waliwekwa kifua mbele kunako dakika ya 23 kupitia kwa mshambuliaji matata raia wa Burundi, Jules Ulimwengu.

Hata hivyo, Belouizdad walirejea mchezoni katika dakika za mwisho huku wakisawazishiwa na Amir Sayoud katika dakika ya 72 kabla Abdelkader Belharane kutoka benchi na kufunga bao la pili katika dakika ya 83.

Maandalizi ya Gor Mahia kwa minajili ya michuano ya mikondo miwili dhidi ya Belouizdad yalitawaliwa na pandashuka tele huku wachezaji wakigomea mazoezi kwa madai ya kutolipwa mishahara na marupurupu.

Chini ya kocha Franck Dumas ambaye ni raia wa Ufaransa, Belouizdad walirejelea kipindi cha pili kwa matao ya juu huku wanasoka Sayoud, Merba na Larbi Tabti wakimweka kipa wa Gor Mahia, Gad Mathews katika ulazima wa kufanya kazi ya ziada.

Licha ya kutamalaki soka ya humu nchini kwa miaka mingi, Gor Mahia wamekuwa wakitatizika kuwika katika soka ta bara Afrika. Wapambe hao wa soka ya Kenya walibanduliwa kwenye kampeni za CAF kwa jumla ya mabao 6-1 mnamo 2019-20 kutoka kwa USM Alger ya Algeria.

Gor Mahia kwa sasa wanatarajiwa kuanza mchakato wa kuajiri kocha mpya atakayejaza nafasi ya Roberto Oliveira ambaye ni raia wa Brazil. Patrick Odhiambo aliyekuwa msaidizi wa Oliveira pia amekatiza uhusiano wake na Gor Mahia.

  • Tags

You can share this post!

Hyvin Kiyeng kuhamia mbio za mita 10,000 na marathon

Wezi wajipikia ugali, nyama na kushukuru familia kwa...