• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Matumaini kaunti ikisaka soko la maembe ng’ambo

Matumaini kaunti ikisaka soko la maembe ng’ambo

NA STEPHEN ODUOR

Serikali ya kaunti ya Tana River imeanza kuweka mikakati itakayoiwezesha kuuza zao la maembe katika masoko ya nchi za kigeni.

Akizungumza katika mkutano wataalamu mbali mbali eneo bunge la Garsen, Gavana wa Tana River Dhadho Godhana alisema kuwa tayari walikuwa katika harakati za kufanikisha mazungumzo na wafanya biashara wa maembe kutoka India na Indonesia.

Bw Godhana alisema kuwa kuna soko la zao hilo katika mataifa hayo mawili, ambayo hukosa maembe katika msimu wa Disemba hadi Februari, wakati ambapo kaunti ya Tana River hushuhudia zao hilo kwa wingi.

Bw Godhana alisema kuwa wakulima katika kaunti huvuna zao kwa wingi, ila mazao hayo huoza katika maghala kwa kukosa soko.

Pia alisema kuwa baadhi ya wanunuzi walikuwa wakiwadhulumu sana wakulima, kwa kununua embe kwa bei rahisi ya kati ya shilingi moja na shilingi mbili, hivyo basi kuwaacha katika hali ya uchochole zaidi.

Alisema kuwa iwapo masoko ya nje yatapatikana, basi ukulima wa maembe utakuwa wa manufaa kwa wakulima, na hivyo kuweka kaunti hiyo katika nafasi ya kipekee kwenye ulingo wa biashara.

‘Tumekuwa tukitegemea sana masoko ya ndani ambayo yametukandamiza sana, ni wakati sasa tupanue akili na mbawa zetu ili tuweze kuonyesha taifa hili kuwa nasi tunaweza kuwa na sauti katika meza ya biashara, ‘alisema

Gavana huyo alisema kuwa mbali na kuwa kuna mashine mpya za uzalishaji sharubati ya maembe, mazao yanayotoka shambani ni mengi kuzidi uwezo wake

Alisema kuwa kuwepo kwa mtambo huo kutaleta nafuu kwa kiasi fulani kwa wakulima.

‘Wakulima wetu huzalisha kiasi cha kumudu kampuni nne za sharubati ambazo hatuna, maembe huenda katika masoko ya Mombasa na Nairobi na bado twasalia na tele kuharibikia shambani, ni heri kupata hela za masoko ya nje, ‘alisema.

Kaunti ya Tana River huzalisha tani elfu thelathini za maembe kila mwaka, huku asilimia arobaini ya zao hilo likiharibika kwenye maghala.

Serikali kwa upande mwengine imewekeza takriban Sh140 milioni kuweza kununua mtambo utakaoweza kusaga tani elfu kumi na mbili za maembe kwa mwaka, huku tani elfu kumi na nane zikikosa soko.

Kaunti ya Tana River huzalisha aina nne za maembe zikiwemo ngowe, dodo, punda na aina ta embe la kipekee lijulikanalo kwa jina maarufu kama Alphonso.

You can share this post!

Muturi na Lusaka wapokea ripoti kuhusu Mswada wa BBI

Karua aonya kuhusu njama ya kuahirisha kura