• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Trump azindua blogu ya kuchapisha taarifa muhimu kutoka kwake

Trump azindua blogu ya kuchapisha taarifa muhimu kutoka kwake

Na MASHIRIKA

WASHINGTON D.C., Amerika

ALIYEKUWA Rais wa Amerika Donald Trump amezindua tovuti mpya ya mawasiliano ambayo itachapisha taarifa zote kutoka kwake.

Trump alisema Jumatatu alichukua hatua hiyo baada ya kupigwa marufuku na mtandao wa kijamii wa Twitter na kusimamishwa kwa muda na mitandao ya Facebook na YouTube.

Hii ni kufuatia madai kuwa Rais huyo wa zamani alichochea fujo katika jumba la Capitol katika kile kilichodaiwa ni jitihada zake za kuzuia Bunge la Wawakilishi kuidhinisha ushindi wa Rais wa Amerika Joe Biden.

Tangu kupigwa marufuku na mitandao hiyo ya kijamii, Trump amekuwa akitoa taarifa zake moja kwa moja kwa vyombo vya habari.

Ni taarifa hizo ambazo sasa tovuti hiyo itakuwa ikichapisha.

Watakaofuatilia taarifa za Trump kutoka kwa tovuti hii, watakuwa wakiruhusiwa kuyaidhinisha na kuzisambaza katika akaunti zao za Twitter na Facebook.

Hatua hiyo ya Trump inajiri siku moja kabla ya Bodi ya Usimamizi ya Facebook kufanya uamuzi ikiwa itamzima kabisa Rais huyo wa zamani au la. Ikiwa ataruhusiwa, basi akaunti yake itafufuliwa.

Mshauru mkuu wa Trump Jason Miller awali alikuwa amedokeza kuwa wangeanzisha mtandao mpya wa kijamii. “Mtandao huu utakuwa kubwa zaidi,” akasema Miller mnamo Machi 2021.

Lakini Jumanne Miller alifafanua kuwa tovuti hiyo mpya sio mtandao wa kijamii ambao aliahidi mwezi Machi.

“Tutatoa maelezo zaidi kuhusu suala hilo siku chache zijazo,” akaeleza.

Inasemekana kuwa tovuti hiyo imetengenezwa na kampuni ya kidijitali kwa jina, Campaign Nucleus, iliyoasisiwa na aliyekuwa meneja wa kampeni za Trump Brad Parscale.

Mtandao wa YouTube ulisema kuwa utafufua akaunti ya Trump wakati ambapo hatari “ya vitisho vyake vya kusabisha fujo itapungua,”

Hata hivyo, Twitter ambako Trump alikuwa na wafuasi milioni 88 ilisema suala la kumzima “ni kitu kilichokamilika.”

Tafsiri: CHARLES WASONGA

You can share this post!

Mwathi achaguliwa mwenyekiti wa kamati ya usalama bungeni

Kocha Koeman atoa orodha ya wachezaji sita anaotaka...