• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 3:55 PM
Madaktari wataka afya iwe ajenda ya mazungumzo

Madaktari wataka afya iwe ajenda ya mazungumzo

NA HELLEN SHIKANDA

WAHUDUMU wa afya, kupitia viongozi wa vyama vya kutetea masilahi yao, wanataka changamoto zinazokumba sekta ya afya zijumuishwe katika mazungumzo kati ya serikali na upinzani.

Wakiongea na wanahabari jana viongozi wa Chama cha Madaktari Nchini (KMPDU) na wenzao wa chama cha maafisa wa kliniki walisema huduma za afya haziwezi kutenganishwa na gharama ya maisha.

Katibu Mkuu wa KMPDU Dkt Davji Atellah alisema kutojumuishwa kwa ajenda ya afya katika mazungumzo hayo kutakuwa sawa na kuweka kando mpango wa Afya kwa Wote (UHC) ambao tayari umesambaratishwa.

“Licha ya ahadi za kila mara, sasa ni wazi kuwa mpango wa UHC unasalia ndoto ambayo umekumbwa na changamoto zinazofanya utekelezaji wake kuwa ngumu,” akasema.

“Tunajua kuwa Wakenya wengi hawawezi kumudu kulipa bili zao za hospitali kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha. Changamoto hii ingepunguzwa na mpango wa afya kwa wote endapo utekelezaji wake ungefanikishwa,” Dkt Atellah akaongeza.

“Ni kinaya kwamba huku hospitali za umma zikikumbwa na uhaba mkubwa wa madaktari, Kenya inaonekana kuendeleza sera ya kufunza na kutelekeza. Aidha, kuna uhaba mkubwa wa maafisa wa matibabu, wafamasia na wataalamu wa meno katika hospitali za umma na wanachama wetu wanalazimika kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupata nafasi ya kupumzika,” akaongeza Dkt Atellah.

Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa wa Kliniki Nchini (KUCO), Peterson Wachira, aliongeza mafanikio ya ugatuzi yaliyotajwa wakati wa kongamano la ugatuzi hayajashuhudiwa katika sekta ya afya.

“Hadithi za ufanisi zilizotolewa katika Kongamano la Ugatuzi mjini Eldoret wiki jana zilishangaza. Kama watu walio mashinani na mashahidi wa yale yanayofanyika katika sekta ya afya katika ngazi za kaunti, tunashangaa ikiwa yale yaliyosemwa yanaakisi hali halisi,” akasema.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Wachira alisema taifa halijatimiza masuala muhimu yaliyojadiliwa 2013 kabla ya harakati za kugatua sekta ya afya kuanza. Miaka 10 baadaye, malengo matano yaliyowekwa katika Mkutano wa Shirika la Afya Duniani kuhusu Wahudumu wa Afya jijini Recife, Brazil, hayajatekelezwa.

Kenya iliahidi kuunda Kamati Shirikishi ya Wahudumu wa Afya katika ngazi za Serikali ya Kitaifa na Serikali za Kaunti, kuajira wahudumu 12,000 wa afya kila mwaka, ushirikishwaji wa wahudumu wa afya ya jamii, kuongeza bajeti ya sekta ya afya na ushirikiano kati ya sekta za umma na za kibinafsi.

Lakini Wachira alisema wahudumu wa afya ya kijamii hawawezi kufanya kazi bila usaidizi wa wafanyakazi wengine muhimu kama vile madaktari, maafisa wa kliniki na wauguzi.

  • Tags

You can share this post!

Vichapo vyatoa pumzi Man United na Chelsea

Barua ya mwisho Joseph Murigi aliandikia mkewe kabla ya...

T L