• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Ardhi jirani na ya Ruto yanyakuliwa Taita

Ardhi jirani na ya Ruto yanyakuliwa Taita

NA WAANDISHI WETU

MZOZO umeibuka katika eneo la Jipe, Kaunti ya Taita Taveta baada ya mwekezaji wa kibinafsi kudaiwa kunyakua takriban ekari 900 za ardhi ya umma inayopakana na shamba la Rais William Ruto.

Wakati huo huo, wanamazingira katika Kaunti ya Kilifi wamelalamikia unyakuzi wa ardhi kwenye mlango wa Mto Sabaki, ikiwemo misitu ya mikoko.

Katika Kaunti ya Taita Taveta, serikali ilikuwa imetenga sehemu ya ardhi husika kutumiwa na wanyamapori kutoka mbuga ya Tsavo Magharibi kufikia Ziwa Jipe wakati wa kiangazi. Sehemu nyingine ilipangiwa kugawanyiwa maskwota walioishi hapo, chini ya mpango wa makazi wa Jipe.

Diwani wa zamani wa wadi hiyo, Bw Reuben Ole Tiges, alidai kuwa shamba hilo limenyakuliwa na mwanasiasa mashuhuri.

“Ikiwa ardhi ilikuwa tupu basi ingerudi mikononi mwa wananchi badala ya mwekezaji kuichukua. La kushangaza ni kuwa wananchi hawakuhusishwa ilihali ardhi hii ni mali ya umma,” akasema.

Viongozi wa kaunti hiyo wakiongozwa na Gavana Andrew Mwadime, wanapanga kufanya mkutano katika eneo hilo ili kutafuta mbinu ya kurudisha ardhi hiyo mikononi mwa wananchi.

Bw Mwadime alionya wanyakuzi wa ardhi dhidi ya kumezea mate eneo hilo na kusema kuwa serikali yake haitakubali eneo hilo kunyakuliwa.

“Wasidhani eti kuna ardhi ya bure Taita Taveta. Wale wanaofikiri wataonea wenyeji wajue viongozi tuko macho,” akasema.

Aliwataka wenyeji kudumisha amani ili kuwapa viongozi nafasi ya kutatua shida hiyo.

Taifa Leo ilibaini kuwa ardhi hiyo ilitwaliwa na serikali mwaka wa 1999. Serikali iliinunua kutoka kwa aliyekuwa Mbunge wa Taveta, Bw Basil Criticos.

“Baada ya kuwatengea wenyeji sehemu ya ardhi hiyo, serikali ilitenga sehemu iliyokuwa imepakana na mbuga kuwa ya uhifadhi,” akasema Diwani wa Wadi ya Mata, Bw Isaac Matolo.

Kuanzia Disemba 2022, mwekezaji alianza kuchimba visima na kuweka sorovea ili kuweka mipaka ya ardhi hiyo.

Hata hivyo, wenyeji waliokuwa na hasira walikata nguzo za kujenga ua wa umeme shambani humo.

Mmoja wa waathiriwa, Bw Simon Solonga, aliitaka serikali kuweka bayana mwekezaji anayefanya ujenzi kwenye kipande hicho cha ardhi.

“Haiwezekani kuwa serikali haijui kinachoendelea hapa. Tunachotaka serikali na mnyakuzi husika wajue ni kuwa hatutakubali ardhi yetu kunyakuliwa,” akasema.

Mkazi mwingine, Bw Peter Makovu, alisema wamekuwa wakiishi kwa amani na kuhofia kuwa mzozo huo utaathiri maisha yao.

“Nimezaliwa hapa na sina mahali pa kuishi. Mimi bado ni skwota,” akasema.

Katika Kaunti ya Kilifi, imebainika mmoja wa wawekezaji wa kibinafsi anadai umiliki wa ekari 60 za ardhi inayopakana na Mto Sabaki. Sehemu ya ardhi hiyo ni misitu ya mikoko iliyofika hadi ziwani, huku ekari takriban 18 ikiwa ni eneo oevu linalotunza mazingira ya mtoni.

Mwenyekiti wa Shirika la Uhifadhi na Ustawishaji wa Mto Sabaki, Bw Joseph Mangi, alisema walishtuka walipopata watu wakikata misitu ya mikoko ili kujenga barabara.

Kulingana naye, imebainika ardhi hiyo imesajiliwa kwa jina la kampuni ambayo inadai ilipewa hatimiliki na serikali.

  • Tags

You can share this post!

Raila atorokwa zaidi na wabunge wa ngome yake ya Luo...

Gavana Nyong’o adai Jalang’o na wenzake 8...

T L