• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:01 PM
Barobaro aeleza jinsi alivyofaidika na elimu bila malipo

Barobaro aeleza jinsi alivyofaidika na elimu bila malipo

NA WANDERI KAMAU

BAROBARO Kioko Mwinzi ni miongoni mwa maelfu ya vijana ambao walinufaika pakubwa kutokana na Mpango wa Elimu Bila Malipo (FPE) alioanzisha Rais Mstaafu Mwai Kibaki mnamo 2003.

Barobaro huyo ambaye anatoka katika eneo la Matuu, Kaunti ya Machakos, anasema kuwa ni kutokana na mpango huo, ambapo alifaulu kwenda katika shule ya msingi, licha ya kiwango kikubwa cha umaskini kilichokuwa katika familia yao.

Kwenye mahojiano, alisema kuwa kinyume na wanafunzi wengine, alijiunga na Darasa la Kwanza akiwa na umri wa miaka 11.

“Kimsingi, wanafunzi wengi hujiunga na Darasa la Kwanza wakiwa na kati umri wa miaka saba au minane. Mimi nilikuwa nimewazidi kwa umri. Ilinilazimu kukaa kivyangu, kwani ilikuwa vigumu kutangamana nao,” akasema barobaro huyo.

Anasema kuwa ili kudhihirisha jinsi mpango huo uliwasaidia watu wengi, zaidi ya nusu ya wanafunzi hawakuwa na sare za shule.

“Wanafunzi wengi walikuwa wakifika shuleni jinsi walivyokuwa ili kusoma. Kando na kutokuwa na sare za shule, wengi hata hawakuwa na chakula. Isingekuwa ni mpango huo, singefaulu kusoma,” akasema.

Barobaro huyo alipita Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) ambapo alizoa alama 358 na kujiunga na Shule ya Upili ya Wavulana ya Lenana.

Baada ya hapo, alipita mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) ambapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Masinde Muliro, alikosomea masuala ya utaalamu wa tarakilishi.

Kwa sasa, barobaro huyo ni mwalimu baada ya kufuzu chuoni mnamo 2019.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Vyama vinavyowapunja wawaniaji vinafaa...

Walilia serikali ishukishe bei ya bidhaa za chakula

T L