• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Facebook yaomba radhi baada ya huduma kupotea

Facebook yaomba radhi baada ya huduma kupotea

Na WANDERI KAMAU

AFISA Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Facebook, Mark Zuckerberg, Jumanne aliomba msamaha kwa watumiaji wa mtandao huo, baada ya kupotea kwa karibu saa sita katika sehemu mbalimbali duniani Jumatatu.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram na WhatsApp waliachwa kwenye mshtuko baada ya huduma hizo kupotea ghafla katika hali tatanishi.

Maelfu ya Wakenya ambao hutumia mitandao hiyo ni miongoni mwa mamilioni ya watu kote duniani walioathirika.

Hapo Jumanne, Bw Zuckerberg alieleza masikitiko yake, akisema watu wengi waliathirika pakubwa, ikizingatiwa baadhi yao huitegemea kuendeshea shughuli zao kama biashara.

“Tumerejesha huduma za mitandao ya Facebook, Instagram na Whatsapp. Tunawaomba radhi kwani tunafahamu jinsi ambavyo wengi wenu huwa mnaitumia kuendeshea shughuli zenu,” akasema kwenye taarifa.

Kupitia Twitter, WhatsApp pia iliomba msamaha kwa watumiaji wake, ikisema imeanza kurejesha shughuli zake kama kawaida.

Kulingana na takwimu za kampuni hiyo, karibu watu bilioni mbili waliathirika.

Facebook ni miongoni mwa mitandao inayotumiwa na idadi kubwa sana ya watu kuwasiliana.

Kampuni hiyo ilitaja tatizo hilo kuchangiwa na matatizo ya kimitambo kwenye mashine zake.

“Wahandisi wetu wamebaini sababu ya tatizo hilo na tayari wameanza kulirekebisha,” ikaongeza Facebook.

Baada ya serikali ya Kenya kuifunga nchi kutokana na janga la corona, watu wengi wamekuwa wakitumia mitandao hiyo kuendesha biashara zao.

“Niliwapoteza wateja kadhaa ambao walikuwa wameahidi kununua bidhaa zao kutoka kwangu,” akasema Bi Lilian Kagendo, ambaye ni muuzaji nguo katika Kaunti ya Nairobi.

You can share this post!

Wanafunzi 20,000 waahidiwa vitambulisho

NGILA: Kupotea kwa huduma za Facebook kuwe funzo