• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Japan yashirikiana na Kenya kuzindua kituo cha utafiti wa malaria chuoni MKU

Japan yashirikiana na Kenya kuzindua kituo cha utafiti wa malaria chuoni MKU

NA LAWRENCE ONGARO

SERIKALI ya Japan imesaidia katika hatua muhimu ya kuzindua maabara mpya ya utafiti katika wa malaria katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU).

Hafla hiyo ilihudhuriwa na balozi wa Japan nchini Kenya Bw Okaniwa Ken, Naibu Chansela wa MKU Profesa Deogratius Jaganyi na Pro-Chansela Dkt Vincent Gaitho.

Kituo hicho kitaleta mwelekeo mpya kwa sababu wanafunzi watafanya utafiti zaidi wa maradhi ya malaria ambayo yamekuwa kero katika maeneo mengi nchini na barani Afrika.

Balazi Okaniwa ambaye alizindua kituo hicho kipya chuoni MKU, alisema anasikitika kuona ya kwamba maradhi ya malaria bado ni janga kubwa linaloangamiza watu wengi.

“Iwapo tutazingatia kufanya utafiti zaidi na kupata suluhu ya jinsi ya kuangamiza maradhi hayo, bila shaka maafa yasababishwayo na malaria yatapungua katika sehemu nyingi hapa nchini,” alisema balozi huyo.

Kulingana na mpango huo, kuna ushirikiano baina ya chuo kikuu cha Japan City University, serikali kuu na Kaunti ya Homa Bay ikishirikishwa na shirika la Japan International Cooperation Agency ( JICA) ili kufanikisha mpango huo.

Mpango huo unataka kuhakikisha malaria hasa katika maeneo ya magharibi mwa nchi ya Kenya, yanakabiliwa vilivyo.

Kulingana na mpango uliopo, mradi huo utagharimu takribani Sh450 milioni.

Kati ya fedha hizo, Sh300 milioni zitafadhili miradi ya Kenya huku Sh150 zikiendesha shughuli za Japan.

Kwa upande wake Prof Jaganyi, alipongeza mpango huo akisema unaweka MKU kwa ramani ya ulimwengu kuhusu utafiti.

“Malaria ni changamoto kubwa nchini Kenya na wanaoathirika zaidi ni watoto na wanawake wajawazito,” alisema msomi huyo.

Dkt Vincent Gaitho ambaye ni Pro-Chansela wa MKU naye alisema ni muhimu kuangamiza malaria kwa sababu mtu asiye na afya njema hawezi akatekeleza wajibu wake ipasavyo.

Alisema chuo cha MKU kinastahili pongezi kwa kupata nafasi ya kuweka kituo hicho cha utafiti jambo alilosema litaleta ushirikiano wa karibu kati ya wanachuo wa Japan na wale wa MKU lakini pia wa kutoka kwa vyuo vikuu vinginevyo ndani na nje ya Kenya.

Alisema wanafunzi watapata ujuzi zaidi kwa kufanya utafiti utakaoleta mwelekeo bora wa namna ya kuangamiza malaria.
  • Tags

You can share this post!

Maafisa watibua njama ya wahuni kuteketeza kituo cha polisi

Raila asema mkate wa Kenya Kwanza umeoza

T L