• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Raila asema mkate wa Kenya Kwanza umeoza

Raila asema mkate wa Kenya Kwanza umeoza

KARIM RAJAN Na WINNIE ATIENO

KINARA wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Bw Raila Odinga, amesema hataki kumegewa nusu mkate na serikali ya Kenya Kwanza.

Alisema hayo wakati alifichua kuwa alikuwa amelazwa hospitalini baada ya kuugua homa kali na hiyo ikawa sababu ya kutoonekana kwake kwenye maandamano.

Kwenye mahojiano ya kipekee jana Alhamisi na Taifa Leo, Bw Odinga alisema aliambukizwa na homa kali siku chache zilizopita ndiposa hajakuwa akionekana hadharani.

“Lakini leo nasikia nafuu. Nataka kuambia Wakenya kwamba, Baba yuko salama. Niliugua sana, nilipata homa kali ambayo ilinisababisha kulazwa. Nilitibiwa na daktari wangu. Lakini naendelea vyema na nitapona,” akasema.

Alifichua kuwa, Ijumaa iliyopita alikuwa Pwani ambapo alikaa Malindi na Kilifi kisha akaelekea Mombasa ambapo alikutana na viongozi wa Azimio, wakiwemo magavana, maseneta na wabunge.

Kiongozi huyo wa Chama cha ODM alisema, Jumatatu alirudi Nairobi ambapo alikutana na viongozi wenzake wa Azimio wakiwemo Martha Karua, Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa, Wycliffe Oparanya, George Wajackoyah, Jeremiah Kioni, Mwangi Wa Iria, miongoni mwa wengine.

Mkutano huo ulikuwa wa kuandaa maandamano ya siku tatu ambayo yalianza Jumatano.

Bw Odinga alisisitiza kuwa, kutokuwepo kwake hakujaathiri maandamano na hiyo ni ishara kwamba Wakenya wamejitolea kupinga ongezeko la ushuru.

“Ninataka Wakenya wajue kwamba, maandamano si ya Baba, Martha Karua wala Kalonzo Musyoka. Yanahusu Wakenya ambao wanapinga gharama ya juu ya maisha na ushuru wa kupita kiasi. Yanahusu Wakenya wanaotaabika kwa sababu ya yale yanayofanyikia uchumi wetu. Hii ndiyo sababu raia wako barabarani,” akasema.

Alisema licha ya kuugua, amekuwa akishirikiana kikamilifu na wenzake katika Azimio ambao wako katika mstari wa mbele kuitaka serikali ipunguze ushuru hasa kwa bidhaa muhimu.

Kulingana naye, serikali ya Kenya Kwanza, ikiongozwa na Rais William Ruto, inasisitiza kufanya hali ya maisha kuwa ngumu kwa Wakenya.

“Serikali imekataa kusikiza kilio cha Wakenya. Azimio inafanya maandamano kwa sababu tunasimama na Wakenya. Nina imani kwa kikosi cha Azimio ambacho kinaongoza maandamano katika sehemu mbalimbali za nchi. Si lazima waonekane barabarani lakini wako pamoja na wananchi. Wakenya, hili jambo linawahusu, jitokezeni mpiganie haki zenu,” akaongeza.

Bw Odinga alitaja siku ya pili ya maandamano kuwa nusu fainali, akidokeza maandamano makubwa zaidi leo Ijumaa ambayo aliyataja kuwa fainali.

Wakati huo huo, alisema hajazungumza na Rais Ruto na akasisitiza hana haja kugawana mamlaka na Kenya Kwanza.

“Hajanipigia simu wala mimi kumpigia. Ninataka Wakenya wajue sisi hatuna haja na handisheki jinsi Kenya Kwanza inavyodai. Hatujawahi na hatutawahi kuomba handisheki. Handisheki ni porojo yao… ati watu wa Azimio wanatafuta handisheki na nusu mkate. Hatutaki mkate wao ambao umeoza,” akasema.

Mnamo Jumatano, Rais Ruto alisema yuko tayari kuzungumza na Bw Odinga kuhusu changamoto zinazokumba Wakenya lakini si kuhusu ugavi wa mamlaka.

Lakini Bw Odinga alishuku uaminifu wa rais, akisema amekuwa akiwapa Wakenya ahadi za uongo.

“Hakuna haja kukaa naye kwa mashauriano kwa sababu hawezi kutimiza ahadi zake. Hawezi kuaminika, leo atasema hivi…kesho anasema vingine. Kenya Kwanza ilitulazimisha kuenda barabarani kwa sababu walikataa matakwa yetu matano wakati wa mashauriano ambayo yalitibuka. Wao ndio wa kulaumiwa,” akasema.

“Punda amechoka. Huwezi kuendelea kuwekea Wakenya mizigo, Wakenya wamekataa,” akaongeza.

Naye akiwa Kaunti ya Isiolo, Rais Ruto jana Alhamisi aliwahakikishia Wakenya kuwa serikali itawalinda pamoja na mali zao.

Alimuonya Bw Odinga kwa kutaka kuitumbukiza nchi kwenye machafuko, akiapa kuwa wote wanaozua fujo na uharibifu wa mali watakabiliwa vilivyo.

“Hatutakuruhusu usambaratishe uchumi wetu kwa kutumia ghasia. Kenya ndiyo nchi tuliyo nayo. Ni lazima tulinde kwa kila njia,” akasema Dkt Ruto alipozindua barabara iliyojengwa na Serikali ya Kitaifa.

  • Tags

You can share this post!

Japan yashirikiana na Kenya kuzindua kituo cha utafiti wa...

Mjane wa Kihindi apinga mwanamke wa Kiafrika kurithi mali

T L