• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 5:29 PM
Mshauri wa kijasusi wa gavana alikufa kwa kula sumu – Ripoti

Mshauri wa kijasusi wa gavana alikufa kwa kula sumu – Ripoti

NA GEORGE ODIWUOR

MSHAURI wa masuala ya ujasusi wa Gavana Gladys Wanga wa Homa Bay, Bernard Omuga, alifariki kwa kula kitu kilichokuwa na sumu, ripoti ya uchunguzi wa maiti imefichua.

Omuga ambaye pia alihudumu kama naibu mkurugenzi wa idara ya utekelezaji, alifariki Jumapili asubuhi katika hali ambayo haikueleweka.
Hii ilikuwa baada ya kujumuika na marafiki na familia yake Jumamosi alasiri katika hoteli moja iliyoko katika kituo cha kibiashara cha Rodi Kopany. Ilifichuliwa kuwa alimeza kitu kilichosababisha kifo chake.

Uchunguzi wa maiti yake uliofanywa Jumatatu katika mochari ya Med 25 iliyoko Kirindo, ulionyesha kwamba mwili wa Omuga huenda ulikuwa na sumu. Watu wa familia yake na maafisa kutoka Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) walishuhudia upasuaji wa mwili.

Dkt Kevin Osuri, aliyefanya upasuaji huo, alisema sampuli zilitolewa katika mwili na kupelekwa maabarani kwa uchunguzi zaidi.
“Tunajaribu kutambua chanzo cha kifo na ripoti iliandaliwa. Lakini ili kuwa na uhakika zaidi kuhusu kilichosababisha kifo, tulituma sampuli kwa uchunguzi zaidi,” alisema.

Daktari huyo alisema sampuli zilitolewa kutoka kwa tumbo, ini, mkojo na damu na pia sehemu za mwili. Dkt Osuri alisema sampuli hizo zilipelekwa katika maabara ya mwanakemia wa serikali kwa uchunguzi zaidi kuhusu sumu.

“Tunatarajia kufanya vipimo ili kubaini iwapo kulikuwa na kemikali katika mwili. Tunataka kujua alikula nini,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

KRA yapata Kamishna Mkuu mpya

Kesha za wavuvi kulinda nyavu katika Ziwa Victoria

T L