• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 6:55 PM
Mzozo wa DPP na DCI waanikwa na kesi ya mauaji ya Cohen

Mzozo wa DPP na DCI waanikwa na kesi ya mauaji ya Cohen

Na BENSON MATHEKA

KESI ya mauaji ya bwanyenye kutoka Uholanzi, Tob Cohen imeanika tofauti zinazoendelea kupanuka kati ya Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI), Bw George Kinoti na mwenzake wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bw Noordin Haji.

Tofauti za wawili hao zinaweza kuhujumu kesi za uhalifu nchini ikizingatiwa kuwa ushirikiano wao ni muhimu katika mfumo wa haki.

Bw Kinoti anamlaumu Bw Haji kwa kukataa kumfungulia mashtaka ya mauaji Jaji wa Mahakama ya Rufaa Sankale Ole Kantai anayedai uchunguzi unaonyesha alihusika katika mauaji ya Bw Cohen.

Kulingana na DCI, jaji huyo alikuwa mshirika wa mke wa Cohen, Sarah Wairimu ambaye ameshtakiwa kwa mauaji ya bwanyenye huyo.

Jaji Kantai amepata agizo la mahakama kuzuia DCI kumkamata bila kuagizwa kwa maandishi na DPP.Ofisi ya DPP inasema kwamba baada ya kuchunguza faili ya uchunguzi wa DCI, haikupata ushahidi wa kumhusisha Jaji Kantai na mauaji ya Cohen.

Jukumu la DPP ni kushtaki washukiwa akiridhika kuwa uchunguzi wa polisi unatosha kuthibitisha kesi kortini. Kulingana na katiba, kazi ya DCI, ambayo ni idara ya uchunguzi wa Jinai ya Huduma ya Polisi, ni kuchunguza kesi na kuwasilisha faili kwa DPP aliye na mamlaka ya kufungua mashtaka.

Kesi ya Cohen, ni moja ya kadhaa ambazo DCI na DPP wamekuwa wakitofautiana.Mnamo Machi 2020, wawili hao walitofautiana kuhusu kushtakiwa kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari ya Kenya, Daniel Manduku aliyeshukiwa kutumia vibaya mamlaka ya ofisi yake katika utoaji wa tenda.

DCI ilimkamata Bw Manduku na kumfikisha kortini Nairobi lakini mahakama ikakataa kutambua karatasi ya mashtaka yaliyoidhinishwa na Bw Kinoti.Mawakili wanasema kuwa hakufai kuwa na vita vya ubabe kati ya DCI na DPP kwa kuwa hawana mamlaka sawa.

“DPP anaweza kuagiza polisi kupitia Inspekta Jenerali kufanya uchunguzi kuhusu suala fulani lakini DCI, iliyo chini ya polisi haiwezi kuagiza DPP kufanya kazi yake ya kushtaki washukiwa. DPP anaweza kurudisha faili kwa polisi lakini DCI haiwezi kulazimisha DPP kufungua mashtaka. Hii ni kwa kuwa kesi ikishindwa, huwa ni kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha na ni DPP anayelaumiwa,” asema Wakili Isaac William Nderitu.

Anasema ushirikiano wa DPP na DCI ni muhimu kwa kufaulu kwa kesi za uhalifu kortini. “Mvutano wa wawili hao ni pigo kwa Wakenya wanaowategemea kupata haki. Ni pigo kwa kesi za uhalifu wa kiuchumi ambazo zinafanya nchi kupoteza mabilioni ya pesa.

“Utafanya washukiwa kuwa na ujasiri zaidi. Wawili hao wanafaa kushirikiana kwa kuwa wanahudumia serikali moja na wanafaa kuwajibika kwa raia,” asema.

Ingawa tofauti zao zimekuwa zikijitokeza hadharani, wawili hao wamekuwa wakikanusha kuwa kuna uhasama na mvutano kati yao. Mnamo Machi mwaka jana, waliambia mkutano wa wanahabari kwamba tofauti kati yao ni za kubuniwa na hazitaathiri utendakazi wao.

You can share this post!

Waislamu waenda Saudia kwa Umrah

TAHARIRI: Sekta ya elimu yahitaji mageuzi