• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Nitakupa kiti cha Kiongozi wa Upinzani ndio uache maandamano, Ruto aambia Raila

Nitakupa kiti cha Kiongozi wa Upinzani ndio uache maandamano, Ruto aambia Raila

NA WYCLIFFE NYABERI 

Rais William Ruto amemwambia kinara wa ODM Raila Odinga kuwa yuko tayari kumbunia afisi rasmi ya Kiongozi wa Upinzani ikiwa hilo ndilo litamfanya asitishe maandamano dhidi ya utawala wake.

Dkt Ruto vile vile, ameshikilia kwamba hakuna nafasi ndani ya serikali yake kwa viongozi wa upinzani kugawana mamlaka, yaani Nusu Mkate.

Badala yake, Rais ameambia  upinzani utekeleze majukumu yake kwa kuikosoa serikali inapofanya maamuzi au kuleta sera mbovu inavyohitajika kisheria.

Kwenye ziara yake Agosti 25, 2013 eneo la Gusii, Dkt Ruto alisema hakuna sababu za mrengo wa upinzani kuitisha maandamano ya uasi dhidi ya utawala wake akisema hata mawaziri wake walikuwa wakiitwa bungeni kuhojiwa kuhusu masuala muhimu ya utawala wake.

“Nimerahisisha kazi yao. Nimewaambia tutengeneze ofisi ya Kiongozi wa Upinzani ambapo mtakosoa serikali kutoka asubuhi hadi jioni mradi msitishe maandamano ya kuharibu mali,” Dkt Ruto aliambia makutano wa Nyamasege, katika eneobunge la Bomachoge Chache.

Dkt Ruto aliongeza, “Mimi naheshimu watu wa upinzani. Wako na majukumu ya kikatiba ya kuhakikisha kwamba serikali imefanya kazi na kutekeleza miradi vilivyo. Hiyo ni kazi waliyopewa na katiba lakini katiba hiyo haiwaruhusu kuitisha maandamano ya kuleta fujo na kuharibu mali.”

Dkt Ruto alisisitiza Wakenya walitoa uamuzi wao kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka uliopita na ni sharti matokeo ya uchaguzi huo yaheshimiwe.

Alionya viongozi dhidi ya kujihusisha kwenye ufisadi akisema mkono wa sheria utawaandama mafisadi wote na hawatakuwa na pahala pa kujificha.

Kiongozi wa taifa aliambia raia kwamba serikali yake ina mpango kabambe wa kushusha gharama ya maisha kwa kuwapa wakulima pembejeo za fatalaiza ya bei nafuu na kubuni nafasi za ajira nchini.

Aliwaambia vijana kuwa watapata nafasi za kazi pindi ujenzi wa nyumba nafuu utakapoanza.

Hivyo, Rais aliwaomba vijana kumakinika na kukoma kujihusisha katika unywaji wa pombe haramu ili ujenzi huo utakapoanza, wafaidi kutokana na kazi hizo.

Aliwaamuru machifu na maafisa wote wa serikali kuhakikisha wamefaulisha vita dhidi ya pombe haramu.

Rais alisema kabla ya kutamatika kwa mwaka huu, atazindua ujenzi wa vyumba 3,000 eneo la Gusii ambavyo bei yake ya kuvimudu itakuwa nafuu.

Katika ziara hiyo leo, Dkt Ruto alikagua miradi ya ujenzi wa barabara zitakazowekwa lami na masoko ya kisasa.

Alianzia ziara yake katika eneo la Nyamasege (Bomachoge Chache), akaenda Nyansiongo (Borabu), Ekerenyo (Mugirango Kusini) na Sironga (Mugirango Kusini).

Dkt Ruto alisindikizwa katika ziara yake ya Gusii na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu, magavana Simba Arati (Kisii) na Amos Nyaribo (Nyamira) na wabunge kadhaa.

Ziara ya jana ya Rais eneo la Gusii ilikuwa yake ya pili chini ya wiki moja. Jumapili iliyopita, alizuru Kaunti ya Kisii alipohudhuria maombi ya pamoja ya madhehebu mbali mbali katika eneo la Nyanturago.

  • Tags

You can share this post!

Muuzaji mitishamba akamatwa kwa kuuza dawa zilizopigwa...

Trump abebwa kama mhalifu wa kawaida baada ya kujisalimisha

T L