• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 3:12 PM
Ogina Koko alenga kuwa Rais akiahidi kuondoa Januari kwenye kalenda

Ogina Koko alenga kuwa Rais akiahidi kuondoa Januari kwenye kalenda

MSANII na mtangazaji maarufu nchini Ogina Koko amedai kuwa ndiye atakuwa Rais wa Kenya ifikapo mwaka 2044.

Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Ogina amewataka washindani wake kujiandaa ili kukabiliana naye hatika kinyanganyiro hicho kikali.

Kwa upande wake anaona heri awanie urais 2044 badala ya 2027 kwani ifikapo wakati huo, anaamini atakuwa ametengeneza hela za kutosha kufanyia kampeni.

“Nitakuwa nimetengeneza hela nyingi kama njugu na kumilki magari ya kifahari kuzunguka katika kila sehemu ya nchi kutafuta uungwaji mkono,” akasema.

Katika manifesto yake, kwanza ataondoa mwezi wa Januari katika kalenda ili kuwaepushia Wakenya mahangaiko ya jua kali la Januari, kila mwaka.

Badala yake, atagawanya mwezi wa Desemba mara mbili yaani ‘Lower December’ na ‘Upper December’.

“Huo utakuwa ndio mwisho wa Wakenya kulialia kila mwanzo wa mwaka,” akasema.

Aidha amesema mara tu baada ya kula kiapo kama Rais, atabadilisha maisha ya Kenya kwa kuhakikisha wafanyikazi wanafika kazini mapema.

Chai itaandaliwa Kericho, kisha ielekezwe kwa paipu hadi Molo kuongezewa maziwa halafu kila boma nchini litawekewa ‘dispenser’ ya chai.

“Sasa kazi ya Wakenya itakuwa ni kufungulia  mifereji ya chai ambayo itaanza saa kumi na moja asubuhi hadi saa tano asubuhi,” akasema.

Ogina amekuwa ni mwanamuziki na mchekeshaji kwa siku nyingi, hii ikiwa ni kabla ya kuzamia taaluma ya uanahabari.

Kwa upande mwingine mifereji ya chai itaendelea kufanya kazi baina ya saa 5.00 asubuhi hadi saa 11.00 asubuhi.

Kuanzia hapo chai itakatika na mifereji ya kupitisha pombe itaanza saa mbili usiku.

Mapipa ya pombe yatasafishwa ili mkondo wa kusafirisha chai uendelee siku ifuatayo.

Ajenda  ya tatu katika manifesto yake atafanya marekebisho makubwa katika sekta ya elimu kwa kuwakabidhi vyeti wale walioshindwa kumaliza masomo ya shule za msingi na upili.

Hii itawasaidia kujihisi kuwa wamekanyaga darasani na kutaalamika.

“Kama mke wako aliachia masomo darasa la nane na wewe darasa la nne nitajumlisha miaka minne na minane ili nipate miaka 12, hii itamaanisha nyote  mtakuwa mmefika kidato cha nne,”

Anasema aliyeachia masomo darasa la nne atakabidhiwa chapa ya cheti(photocopy), huku aliyefika darasa la nane akipatiwa cheti halisi(original).

Ogina Koko vilevile anaamini kuwa ndiye ataibuka mshindi katika kinyanganyiro cha kiti cha urais 2044. Lau sivyo Kenya itauzwa na kila mtu apate pesa zake aende sehemu ambayo anataka.

  • Tags

You can share this post!

El Nino huenda isigonge Nyeri sana, mtaalamu afichua

Wanaoishi na HIV kupata dawa za kupunguza makali kwa bei...

T L