• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Ondoa gharama ya kununua fatalaiza kwa kujitengezea mbolea asilia na yenye rutuba

Ondoa gharama ya kununua fatalaiza kwa kujitengezea mbolea asilia na yenye rutuba

Na SAMMY WAWERU

TIMOTHY Mburu ni mkulima wa mseto wa mimea eneo la Gitinga, Naromoru, Kaunti ya Nyeri.

Hukuza mimea kama vile viazimbatata, kabichi, vitunguu, maharagwe asilia maarufu kama minji na mboga aina ya sukuma wiki na spinachi.Aidha, ni mkulima wa mashamba makubwa mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 10.

Katika jitihada zake kuimarisha shughuli za kilimo, Mburu anasema hajaepuka mjeledi wa kero ya pembejeo duni.“Kuna fatalaiza nyingi zilizosheheni katika soko la bidhaa za kilimo na ambazo hazijaafikia ubora,” Mburu anasema.

Ni kero ambayo imechangia wakulima wengi kukosa kuafikia matamanio yao, wakiishia kukadiria hasara bin hasara.Kulingana na mkulima Mburu, kabla agundue siri ya kukwepa changamoto hiyo, aliishi kuwa mtumwa wa mbolea duni, anayotaja haina virutubisho vya kutosha na madini.

“Maandishi unayoona katika baadhi ya mifuko yakisifia bidhaa, ni kwa minajili ya kunogesha mauzo. Hayana virutubisho wala madini yaliyoandikwa,” aeleza. Taswira hiyo si tofauti kwa dawa na pia mbegu.  Hata ingawa hajaasi ile ya madukani, ndiyo fatalaiza, Mburu anasema aligundua siri ni kujitengenezea mbolea.

Ni mfugaji wa kuku, mbuzi, kondoo na ng’ombe, na samadi ya mifugo wake huitumia kuunda mboleahai, anayosema ana uhakika wa virutubisho.“Huichanganya na majani na matawi, na malighafi yanayotumika katika utengenezaji wa fatalaiza yenye madini faafu,” Mburu anadokeza.

Picha/ Sammy Waweru.
Mkulima Paul Nyota (kushoto) na mfanyakazi wake wakionyesha mbolea asilia ya kujitengenezea.

Hufunika mchanganyiko huo kwa muda wa miezi kadhaa, kati ya miezi mitatu hadi sita, ili mbolea iive sambamba.Muda huo pia husaidia kuua viini visababishi vya magonjwa na pia wadudu walio kwenye kinyesi cha mifugo, majani na matawi.

Ubunifu huo wa kipekee pia umekumbatiwa na Paul Nyota, ambaye ni mkulima eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu.Wakulima hawa kwa kauli moja wanakiri hatua hiyo imewasaidia kupunguza gharama kwa kiwango kikubwa.

“Ninapofanya shughuli za utunzi hutumia mboleahai, ninayotengeneza kwa kutumia samadi ya mifugo na majani na matawi,” Nyota anasema.Isitoshe, mkulima huyu wa mseto wa mboga, pilipili mboga, nyanya, matunda na vitunguu, pia hutumia mbolea anayounda kuboresha mazao.

“Huichanganya na ya madukani, na ambayo nina uhakika nayo,” aeleza.Huku kilimo cha Mburu na Nyota kikiwa biashara, wanasema mfumo wa kujitengezea mbolea asilia ukikumbatiwa na wakulima wengine kiwango cha mapato kitaongezeka.

“Unapofunika mchanganyiko wa mbolea, uupe muda kiwango cha Nitrojini huongezeka,” Mburu ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya kilimo anafafanua.Mdau huyu anahimiza wakulima kutumia kwa wingi majani na matawi ya maharagwe, baada ya mavuno, kufanikisha shughuli hiyo.

“Mharagwe yanaorodheshwa katika Familia ya Legumi, ambayo imesheheni Nitrojini, madini muhimu sana katika kilimo,” anasema.Kando na kupunguza gharama katika kilimo, mbolea asilia ya kujitengenezea ni hai na inayodumisha kigezo cha kilimohai.

Uzalishaji wa mazao kwa kutumia fatalaiza na dawa zenye kemikali, umehusishwa na ongezeko la visa vya Saratani na maradhi mengine ya lishe.Ni muhimu kukumbusha mkulima, matumizi ya fatalaiza za aina hiyo huchangia kemikali kusalia udongoni.

Kemikali ni kiini kikuu cha udongo kuwa hafifu, kutokana na kupungua kwa rutuba.“Kinachochangia udongo kupunguza na kupoteza rutuba kabisa ni kuendelea kutumia dawa na fatalaiza zenye kemikali.Wakulima warejelee mifumo asilia ya matumizi ya mboleahai, kama vile ya mifugo kuendeleza kilimo ili tudumishe ubora wa udongo,” anahimiza David Kariuki, afisa na mtaalamu wa kilimo Kaunti ya Kirinyaga.

Picha/ Sammy Waweru.
Paul Nyota, mkulima eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu anasema huunda mbolea kwa kutumia samadi ya mifugo, majani na matawi, hatua anayosifia kumpunguzia gharama.
  • Tags

You can share this post!

Takataka iliyowakera wakazi eneo la viwandani na mtaani wa...

Masika na timu yake ya Vissel Kobe waaga Levain Cup