• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Rai Serikali ihifadhi vyumba vya mateso Nyayo kama kumbukumbu ya kihistoria

Rai Serikali ihifadhi vyumba vya mateso Nyayo kama kumbukumbu ya kihistoria

NA KENYA NEWS AGENCY

MAKUNDI ya mashirika ya kijamii na wahanga waliopitia mateso katika vyumba vya Jumba la Nyayo, Alhamisi waliadhimisha miaka 20 tangu dhuluma hizo kutangazwa kama aibu kubwa katika historia ya humu nchini.

Maadhimisho hayo yalianza Februari 2003 na yamekuwa yakifanywa kila mwaka.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kutetea haki za kibinadamu nchini (KHRC), Bw Davis Malombe, alisema shirika hilo, liliwasilisha ombi kwa Waziri wa Usalama, Prof Kithure Kindiki, likitaka ilani ya gazeti rasmi la serikali nambari 11 ya mwaka 1991, iliyotawaza vyumba vya chini ya Jumba la Nyayo kama eneo lenye ulinzi mkali, kufutiliwa mbali.

Akiongea wakati wa maadhimisho ya mwaka huu katika Jumba la Nyayo, Nairobi, Bw Malombe alisema kuwa orofa ya chini ya jumba hilo na orofa za 24, 25, 26 zinafaa kuwa eneo la kumbukumbu.

“Vyumba vya Mateso vya Nyayo vinapasa kuwa eneo la kumbukumbu na mafunzo. Hii ni mojawapo ya mapendekezo ya Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano (TRJC),” akasema Bw Malombe.

Alitoa wito kwa serikali ya sasa kutimiza ahadi iliyotoa wakati wa mazishi ya shujaa wa uhuru Mama Mukami Kimathi ya kufukua mabaki ya shujaa Dedan Kimathi ili kuyapa mazishi ya kiheshima.

Bw Malombe pia alitoa wito kwa serikali kuanzisha hazina ya Urejeleaji wa Haki ya Sh10 bilioni, katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024.

Hazina hiyo ililenga kuwasaidia manusura na wahanga wa dhuluma za kihistoria. Kwa upande wake Katibu wa Shirika la Kitaifa la Wahanga wa Mateso (NVSN), Bw Wachira Waheire, alisema kuwa historia ya taifa hili haifai kusahauliwa.

“Hatuwezi kuwasahau wazalendo wa taifa hili ambao waliteswa na kuuawa ndani ya vyumba vya mateso,” akasema Bw Waheire.

Alisema juhudi za wafungwa wa kisiasa na wahasiriwa wengine ndizo zilichangia kuondolewa kwa Sehemu ya 2A ya katiba ya zamani na kupatikana kwa Katiba ya 2010.

Bw Waheire alitoa wito vijana nchini kujihusisha zaidi katika masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi huku akiwakumbusha uhuru wanaofurahia sasa ulitokana na mateso kwa binadamu. Alilaani madai ya kuharibiwa kwa vyumba vya mateso vya Nyayo, akiitaja kama kitendo cha kuvurugwa kwa historia ya taifa la Kenya.

“Tunawakumbuka Wakenya wazalendo walioteswa na kuuawa , waliojitia kitanzi, waliobakwa na familia zilizovunjika na wapendwa wao kuteseka kwa sababu ya uhuru wa taifa hili,” akasema Bw Waheire.

  • Tags

You can share this post!

Sonko aonyesha kamera za CCTV zilizosheheni kwake akisema...

DOUGLAS MUTUA: Waafrika watafute mbinu za kusuluhisha...

T L