• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:20 PM
RAMADHAN: Kufunga Ramadhani si mateso bali zawadi kwa muumini

RAMADHAN: Kufunga Ramadhani si mateso bali zawadi kwa muumini

Na NUR SAID

ENYI mlioamini imefaradhishwa kufunga juu yenu kama walivyofaradhishiwa waliokuwepo kabla yenu ili muweze kupata uchaji Mungu.

Ayah hii inampa mwanadamu zawadi kubwa sana atakapofunga Ramadhani. Saum ni kujizuia na kula na kunywa na pia kujizuia na matamanio ya nafsi yako. Ni kujizuia na mambo ambayo Mungu amekukukubalia katika miezi mingine ila kwa mwezi huu tu ikawa usiyafanye.

Kwa kukubali mwito huu wa Mungu basi yeye amekuandalia zawadi kubwa sana siku ya kukutana naye.

Anasema Mtume SAW), “Mwenye kufunga siku moja tu kwa ajili ya Mwenyeezi Mungu, Basi Mungu atamweka mbali sana na moto wa jehanamu kadri ya safari ya miaka sabini.”

Hebu jiulize safari ya miaka sabini itakufikisha wapi? Hio ndo itakuwa umbali wako mwenye kufunga na moto. Sasa vipi Saum iwe mateso?

Madaktari wengi tena wakubwa ulimwenguni wamekubaliana ya kwamba mwenye kufunga Ramadhani basi huwa ni miongoni mwa njia za kusafisha mwili wake.

Anapotoka katika funga ya Ramadhani basi mwili wake huwa umejengeka vizuri, umeyatoa magonjwa yote na umejirutubisha sawa sawa.

Na hili pia amelithibitisha Mtume (SAW) aliposema, “Fungeni mtapata afya nzuri.” Kwa hivyo unavoketi njaa mchana kutwa na kasha ukafungua magharibi kwa tende na maji basi ni kirutubisho tosha kwa mwili wako. Hii ni zawadi. Vipi itakuwa ni mateso?

Wenye kufunga wameahidiwa kuwa wataingia peponi kupitia mlango unaojulikana kama Rayyan. Hakuna mwengine atakayeruhusiwa kutumia mlango huo isipokuwa wenye kufunga pekee. Na watakapoingia basi mlango ule utafungwa.

Kama wewe umeshapangiwa mpaka na mlango utakayotumia kuingia peponi kwa ajili tu ya kufunga vipi tena useme ama mtu akwambie funga ya Ramadhani ni mateso? Jivunie na uifunge kwa raha tena kwa uthabiti wa hali ya juu.

Kisha anasema tena Mtume mwenye kufunga Ramadhani kwa imani na kutegemea malipo kutoka kwa mwenyeezi Mungu, atasamehewa madhambi yake yote yaliotangulia. Ina maana inapokwisha Ramadhani wewe utakuwa msafi kama pamba.

Mwisho kabisa yule ambaye atatoa zakatul Fitr katika mwisho wa kufunga zakat kama ile ambayo hutolewa kibaba cha chakula ambacho huliwa sana pale mtaani, inakuwa ni ya kuisafisha saum yake na kuifanya kufika kwa Mungu ikiwa haina madoa.

Zakatul Fitr ni ya kuwawezesha wasiojiweza pia kufurahia Idd yao. Inakuwa ni siku ya furaha kwa kumaliza kufunga kisha inabakia furaha nyengine ya kukutana na Mola wako.

Hiyo ndiyo raha ya funga ya Ramadhani. Asikwambie yeyote kwamba ni mateso. Ni raha na malipo yake ni makubwa zaidi.

You can share this post!

Watatu wafariki lori na matatu zikigongana mjini

Onyo kuhusu mafuriko eneo la Ziwa Victoria