• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:05 PM
USHOGA: Sheria tata yaanza kazi mshukiwa wa kwanza akikodolea macho adhabu ya kifo

USHOGA: Sheria tata yaanza kazi mshukiwa wa kwanza akikodolea macho adhabu ya kifo

NA AFP

KAMPALA, UGANDA

MWANAUME mmoja Uganda anayedaiwa kuwa shoga ameshtakiwa, jambo ambalo huenda likafikia kifo chake chini ya sheria tata nchini humo inayopiga marufuku uhusiano wa jinsia moja.

Sheria hiyo inayochukuliwa kuwa kali zaidi duniani ina vifungu vinavyofanya ushoga kuwa kosa linaloadhibiwa na kifo na hadi kifungo cha maisha jela.

“Mshukiwa alishtakiwa huko Soroti (mashariki mwa Uganda), na yuko rumande. Atafikishwa mahakamani ili kesi yake kusikizwa,” akasema Jacquelyn Okui, msemaji wa ofisi ya mkurugenzi ya mashtaka ya umma nchini Uganda.

Kulingana na hati ya mashtaka, mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 20 alishtakiwa mnamo Agosti 18 na anatuhumiwa kushiriki mapenzi na mwanaume mwenzake wa umri wa miaka 41.

“Kosa lake ni la kushiriki mapenzi na mwanaume mwenzake kinyume na Sheria ya Kupinga Ushoga 2023”, karatasi ya mashtaka ilisoma.

Okui alisema hana uhakika kama hii ni mara ya kwanza raia wa Uganda kushtakiwa kwa kuhusika katika masuala ya ushoga chini ya sheria hiyo mpya.

Adrian Jjuuko, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Uhamasishaji na Ukuzaji wa Haki za Kibinadamu, alisema shirika lake lina ripoti ya kukamatwa kwa watu 17 mnamo Juni na Julai kufuatia kupitishwa kwa sheria hiyo mpya.

Haya yanakuja siku chache baada ya polisi kuwakamata watu wanne wakiwemo wanawake wawili kwa madai ya kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Msemaji wa polisi wa eneo la Ssezibwa, Hellen Butoto alisema wanne hao wanaoshukiwa kuhusika katika mapenzi ya jinsia moja wanafanya kazi katika vituo vya uchuaji wa mwili vya Cloud 9 na Chills Out.

Sheria hiyo kali, ambayo ilitiwa saini kuwa sheria mwezi Mei, inapingwa vikali na Umoja wa Mataifa, serikali za kigeni ikiwa ni pamoja na Amerika na makundi ya kutetea haki za binadamu duniani.

Mwezi huu Benki ya Dunia ilisitisha usaidizi wake kwa taifa hilo, ikisema sheria hiyo kimsingi inakinzana na maadili yanayopendekezwa na Benki hiyo.

Mwezi Mei, Rais wa Amerika, Joe Biden, alitoa wito wa kufutwa mara moja kwa sheria hiyo alitaja kama ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kutishia kupunguza misaada na uwekezaji nchini Uganda.

Lakini serikali ya Uganda imesalia kuwa na msimamo mkali na sheria hiyo inaungwa mkono na wengi katika nchi hiyo iliyo na Wakristo wengi, ambapo wabunge wametetea hatua hizo kama kingo muhimu dhidi ya ufisadi unaohusishwa na Magharibi.

Naye Rais wa Uganda Yoweri Museveni aliishutumu Benki ya Dunia kwa kutumia pesa kujaribu kuishinikiza serikali kutupilia mbali sheria hiyo yenye utata.

  • Tags

You can share this post!

Polisi sasa kuvaa sare mpya

CECAFA: Vihiga Queens kuvaana na Buja Queens kusaka nafasi...

T L