• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Vuguvugu lataka mazungumzo ya maridhiano yafanyike kwa nia njema

Vuguvugu lataka mazungumzo ya maridhiano yafanyike kwa nia njema

NA BENSON MATHEKA

WANASIASA wanafaa kukumbatia mazungumzo ili kuleta maridhiano alivyopendekeza Rais William Ruto ili uthabiti wa kisiasa udumu nchini, vuguvugu la Kuungana, Kujenga na Kusaidia Kenya (KKKK) linasema.

Hata hivyo, vuguvugu hilo linasisitiza kuwa maridhiano yatapatikana iwapo pande zote zitakuwa na nia njema ya kuleta amani, maendeleo na kumaliza ufisadi na ukabila nchini.

Kwenye taarifa, Katibu Mkuu wa KKKK David Waititu Kimengere alisema kwamba ghasia na vitisho hazifai katika kusuluhisha migogoro ya kisiasa kwa kuwa zinavuruga amani na kulemaza uchumi.

“Kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, sisi kama KKKK tuliahidi kufuata mkondo wa kikatiba na kisheria na tukawataka viongozi wengine wa kisiasa kufanya hivyo. Tumekuwa katika nchi hii Kwa miaka mingi na tunajua maridhiano kupitia mazungumzo huzaa matunda mazuri yakifanyika kwa nia njema,” Bw Kimengere alisema.

Alisema kuwa upinzani wa sasa katika serikali sio wa kupuuzwa ikizingatiwa kuwa Rais (Mstaafu) Uhuru Kenyatta anauunga mkono akiwa mwenyekiti wa Baraza Simamizi ya Azimio la Umoja One Kenya.

Katika hali hii, anasema, mazungumzo ya maridhiano hasa kujadili jinsi ya kupunguza gharama ya juu ya maisha inayokumba Wakenya ni muhimu.

“Lazima yahusishe wadau wote kwa kuwa Kenya sio ya mirengo miwili ya kisiasa japo tunaheshimu serikali iliyoko mamlakani,” alisema.

Kupanua mazungumzo kujumuisha matabaka yote, kunaweza kuwa suluhu kwa dhuluma zinazodaiwa kufanyika kila baada ya uchaguzi, ukabila, ufisadi na upendeleo katika serikali.

  • Tags

You can share this post!

Janjajanja za Gachagua kuzima handisheki

Kutengana na Mwamburi hakukumponza gwiji wa rhumba Muyonga

T L