• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 11:29 AM
Wito wa viongozi wa kidini Kisii Rais Ruto na Odinga wapatane   

Wito wa viongozi wa kidini Kisii Rais Ruto na Odinga wapatane  

NA WYCLIFFE NYABERI

BAADHI ya viongozi wa kanisa kutoka Kisii wamezidisha wito wa kutaka Rais William Ruto na kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga kulegeza misimamo yao mikali kuhusu mazungumzo yanayotarajiwa kutatua joto la kisiasa linalozidi kupanda.

Viongozi wa Pentecostal Evangelistic Fellowship of Africa (PEFA)-Kisii wamehimiza wanasiasa waliochaguliwa kufanya upatanishi kwa niaba ya mirengo ya kisiasa ya Kenya Kwanza na Azimio, kujadiliana kwa umakini ili waweze kunusuru nchi dhidi ya machungu zaidi kwa sababu ya siasa.

Akizungumza mwishoni mwa juma wakati wa kulitakasa kanisa jipya la PEFA mjini Kisii, aliyekuwa Askofu mkuu wa kanisa hilo Mophat Kilioba alisema ni wakati sasa viongozi wa kisiasa kuweka kando tofauti zao kwa ajili ya nchi.

“Kenya inatamani amani na ghasia ziepukwe. Kama nchi, tunaomba amani idumu,” Askofu Kilioba alisema.

Semi hizo za wana-PEFA zinajiri siku chache baada ya Rais Ruto kukashifu kinara wa Azimio, Bw Raila Odinga endapo anatarajia kushirikishwa katika serikali anapaswa kusahau kwani Wakenya waliamua 2022 anayepaswa kuwaongoza.

Rais Ruto ameweka wazi kwamba hataitikia maridhiano yanayolenga  kuwepo kwa handisheki au serikali ya nusu mkate.

Dkt Ruto pia ameonya kuhusu maandamano ya upinzani, akisisitiza hatakubali uharibifu wowote wa mali na biashara.

Hata hivyo, Bw Odinga amepuuzilia mbali madai kwamba anatafuta kujiunga na serikali kupitia mlango wa nyuma akitaja serikali ya Kenya Kwanza kama iliyosheheni mafisadi.

Huku kukiwa na msukumo na vuta nikuvute ya kisiasa, kanisa la PEFA limejiunga na madhehebu mengine katika kutoa mwito wa upatanisho kati ya pande hizo kinzani.

“Kama kanisa tulitoa maoni yetu kuhusu haja ya kuunda afisi rasmi ya Kiongozi wa Upinzani ili tusije tukaingia kwenye msururu wa vurugu za kuleta maafa na umwagikaji damu katika mitaa yetu,” alisema Askofu Kilioba.

Maoni yake yaliungwa mkono na mkuu wa askofu wa Nyanza Magharibi, Bw Simeon Mosoti.

Askofu Mosoti alihimiza muungano wa Azimio kufutilia mbali mipango kufufua maandamano, akisikitikia uharibifu wa mali na biashara unaotokana na vurugu.

“Juhudi zote zielekezwe kwenye mazungumzo badala ya kupigana. Kama kanisa tunaunga mkono amani,” alisema.

Kufuatia maandamano ya Azimio, visa kadha vya maafa na majeraha mabaya vimeripotiwa, maafisa wa polisi wakilaumiwa kutumia nguvu kupita kiasi.

 

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Gachagua awataka Wakenya kumuombea Kenyatta kukubali Ruto...

Mwanamume Murang’a aangamiza watoto wake wawili kwa...

T L