• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Kisii: Makanisa, wahubiri kuanza kulipa maelfu kuruhusiwa kufanya kesha na kuendesha Injili mitaani

Kisii: Makanisa, wahubiri kuanza kulipa maelfu kuruhusiwa kufanya kesha na kuendesha Injili mitaani

NA WYCLIFFE NYABERI

BAADHI ya wahubiri na makasisi wanasema hatua ya serikali ya Kaunti ya Kisii ya kuanza kutoza ushuru makanisa na wahubiri itarudisha nyuma injili.

Makanisa yanayofanya maombi ya mkesha wa usiku almaarufu ‘kesha’ yatatakiwa kulipa Sh5,000 kila wiki mara tu Gavana Simba Arati atatia saini Mswada wa Fedha wa Kaunti ya Kisii wa 2023, ambao tayari umepitishwa na Bunge la Kaunti hiyo.

Mswada huo unapendekeza kwamba makanisa yanayotaka kuendesha kesha, yatalazimika kulipa ada hiyo.

Naye mhubiri yeyote atakayeingia mitaani kueneza Injili atalazimika kutenga Sh2,000 kwa wiki ili aruhusiwe kuhubiri.

Ada ni kubwa zaidi kwa wahubiri ambao watatumia magari ya kubebea mizigo yenye vipaza sauti kwa sababu watahitajika kulipa hadi Sh20,000 kwa wiki.

Mara baada ya Mswada huo kupitishwa, baadhi ya makasisi wamejitokeza kulaani hatua ya uongozi wa kaunti kutaka kuwatoza, ilhali hawakuwa wakizilipa miaka iliyopita.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wachungaji na Makasisi wa Kisii Lawrence Nyanuga ametaja uamuzi huo kuwa wa kusikitisha na kumtaka Gavana Simba Arati kutouidhinisha hadi maswala yanayowagusa yatazamwe upya na kufanyiwa mabadiliko.

Kasisi Nyanuga alisema hatua hiyo ni usaliti wa hali ya juu zaidi ambao kanisa eneo la Kisii limepata kutoka kwa viongozi waliochaguliwa, waliokuwa wakiwatembelea wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 kusaka maombi na uungwaji mkono kutoka kwa waumini wao.

“Sasa wametugeuka na wanataka kututoza ushuru. Walipokuwa wakitafuta nyadhifa za uongozi, walikuwa wakituomba tuwaombee na kuwataka waumini kuwaunga mkono,” mchungaji Nyanuga akasema.

Alijutia hatua ya kulitoza kanisa kodi na badala yake akaomba makanisa yaungwe mkono na serikali ili yawezeshwe kufikia nyoyo za watu wengi kwa njia ya uinjilisti.

“Katika hali nyingi, kesha hazivutii watu wengi. Serikali ya kaunti inafikiri kwamba tunapata pesa kwa kufanya mikesha ya usiku lakini sivyo. Makanisa si mashirika ya kutengeneza faida na kwa hivyo hayafai kuchukuliwa vinginevyo,” alisema kasisi Nyanuga.

Huku makasisi hao wakishikilia kuwa kutoza ushuru makanisa ni sawa na kumtoza Mungu ushuru, wakazi wengine wa Kisii wamefurahia wakisema makanisa kulipa ushuru ni njia itakayosaidia kudhibiti wahubiri na makanisa yanayocheza muziki kwa sauti ya juu haswa katika maeneo ya makazi.

“Naunga mkono kikamilifu hatua ya watu wanaoendesha kesha kulipa kodi. Kwa mfano, huwa sipati hata lepe la usingizi siku za Ijumaa katika sehemu ninayoishi kwa sababu ya sauti zinazoshindana kutoka kwa makanisa mbalimbali yaliyo hapo.

“Ninaipongeza Serikali ya Kaunti ya Kisii kwa kuja na pendekezo hilo ambalo kwa maoni yangu lilipaswa kuletwa mapema. Hili likishaanza kutekelezwa, nina uhakika litazima makanisa na maeneo mengine ya ibada kupiga muziki kwa sauti ya juu na hili litanipa fursa nzuri ya kupata usingizi mnono,” akasema Bw Enock Ogoti, mkazi wa kiunga cha Daraja Mbili.

  • Tags

You can share this post!

DCI wasaka genge linalovunja magari na kuiba pesa wateja...

Portland sasa kuuza vipande vitatu vya ardhi yake ikiwapa...

T L