• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Wakazi Kisumu watakiwa kuwa macho kuhusu Kipindupindu

Wakazi Kisumu watakiwa kuwa macho kuhusu Kipindupindu

ELIZABETH OJINA NA PETER CHANGTOEK

KAUNTI ya Kisumu iko katika hali ya tahadhari, baada ya visa vitano vya ugonjwa wa kipindupindu kuripotiwa.

Kwa mujibu wa afisa mkuu wa huduma za afya, Dkt Gregory Ganda, maeneo yaliyoathirika mno ni Nyalenda A and Nyalenda B.

“Idara inafuatilia kwa karibu na kuchunguza visa vinavyoshukiwa vya kuharisha eneo la Kanyakwar Kachok, Capital, Mamboleo, Libeto na Kapuothe,” akasema Dkt Ganda.

Kipindupindu ni ugonjwa wa kuambukizwa, unaosababishwa na bakteria, na husababisha kuhara, kuisha kwa maji mwilini na hata kusababisha kifo.

Bakteria hizo husambaa kupitia chakula na maji machafu, na ni muhimu kuchukua hatua za kukinga ili kuzuia kusambaa.

“Tunawashauri wakazi wote kuwa waangalifu na kudumisha viwango vya juu vya usafi, ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji kabla na baada ya kuingia chooni na kabla ya kula,” alisema.

Wakazi wa Kisumu wameombwa kutia dawa maji au kuyachemsha na kukumbatia utumiaji bora wa vyoo.

Dkt Ganda aliongeza kuwa, serikali ya Kaunti ya Kisumu imechukua hatua za kuzuia mlipuko wa ugonjwa huo, kwa kutoa maji safi ya kunywa na kupikia katika maeneo yaliyoathirika, ili kuimarisha shughuli za usafi.

Aliwaomba wakazi walio na dalili za kipindupindu; kama vile kuendesha sana na kutapika, kupata matibabu katika vituo vya afya vilivyoko karibu.

Aidha, wameombwa kuacha kununua vyakula barabarani na kuhakikisha kuwa vyakula vinapikwa vizuri na kuliwa vikiwa moto.

Mnamo Januari, watu tisa walilazwa katika Hospitali ya Kaunti, Komewa, Seme, wakiwa na ugonjwa wa kuendesha.

Ugonjwa huo wa kipindupindu umelipuka wakati ambapo kaunti jirani ya Kakamega imeripoti kutokea kwa ugonjwa uliosababishwa na maji machafu, na uliosababisha vifo vya wanafunzi watatu wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Mukumu na mwalimu mmoja na wengi kulazwa hospitalini.

 

  • Tags

You can share this post!

Riggy G kuongoza hafla ya utoaji mahari ya mbunge Murang’a

Azimio yapeleka ajenda kwa MCAs

T L