• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
KNEC yakiri kulikuwa na dosari katika matokeo ya KCPE

KNEC yakiri kulikuwa na dosari katika matokeo ya KCPE

NA WINNIE ONYANDO

BARAZA la Mitihani nchini (KNEC) Jumamosi Novemba 25, 2023 lilikiri kulikuwa na dosari katika matokeo ya mtihani wa mwisho wa Darasa la Nane (KCPE) uliotangazwa Alhamisi na Waziri wa Elimu Eekiel Mochogu.

Hii ni baada ya walimu na wazazi kutoka shule mbalimbali kuonyesha kutoridhishwa kwao na matokeo hayo.

Afisa Mkuu Mtendaji wa baraza hilo, David Njengere katika barua alisema kwamba baraza hilo limepokea malalamishi kadhaa kutoka kwa wazazi, walimu na watahiniwa kuhusu matokeo hayo.

“Tumepokea malalamishi kuhusiana na matokeo hayo. Hata hivyo, tumeshughulikia malalamishi 133,” akasema Dkt Njengere.

Kando na hayo, Dkt Njengere alisema kwamba watahiniwa wote watembele shule zao ili kupata nakala ya matokeo ya mtihani na kuwasilisha malalamishi yao ndani ya siku 30.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya wazazi Kuanti ya Meru kuandamana kupinga jinsi mtihani huo ulivyosahihishwa kwa haraka.

Wazazi hao walidai kuwa hatua ya KNEC kuharakisha usahihishaji wa mtihani huo huenda ulichangia dosari nyingi.

Kando na hayo, kuna baadhi ya watahiniwa ambao walipata alama ya Lugha ya Ishara ilhali hawakufanya somo hilo.

Kadhalika, kuna shule ya msingi ambayo kila mtahiniwa alipata alama 75 katika somo la Sayansi.

Naye mtahiniwa Samuel Smith aliyepata alama ya 378 alisema kwamba hakutarajia kupata chini ya 400.

“Mwanangu alipata 378 ila kuna somo moja hakufanya na akawekewa alama ya 68. Kiingereza alipata A (78), KSL B (68), Hisabati A (82), Sayansi B (72), na SSR A (78) jumla ya 378,” akasema Arbigail Timinah, mamake mwathiriwa.

“Mwanangu hakufanya Lugha ya Ishara (KSL) ila akapewa alama ya 68.”

Haya yote yalizua masuala kuhusu jinsi mtihani huo ulivyosahihishwa.

KNEC, hata hivyo, lilisema kuwa itashughulikia suala hilo na kuchukua hatua mwafaka ili kuhakikisha kuwa makosa hayo yameshughulikiwa ipasavyo.

Zaidi ya wanafunzi milioni 1.4 walifanya mitihani huo ulioanza Novemba 30.

Hata hivyo, zaidi ya wanafunzi 9,000 hawakufanya mtihani huo kutokana na changamoto mbalimbali.

  • Tags

You can share this post!

Israeli na Hamas wabadilishana wafungwa na waliokuwa...

Kalameni aangushia mama yake mijeledi akidai anamchafulia...

T L