• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Maafisa wa Kamati ya Makabidhiano ya Afisi ya Gavana wamulikwa kuhusu madeni

Maafisa wa Kamati ya Makabidhiano ya Afisi ya Gavana wamulikwa kuhusu madeni

NA MARY WANGARI

MAAFISA wa Kamati inayosimamia Makabidhiano ya Afisi ya Gavana wamemulikwa kuhusiana na madai ya kupachika bili bandia za malipo hivyo kuongeza mzigo wa madeni yanayolemaza utendakazi na utoaji huduma katika kaunti.

Haya yamejiri huku serikali za kaunti nyingi zikikabiliwa na malimbikizi ya madeni ya mabilioni ya fedha ambazo bado hazijalipwa miezi tisa tangu serikali mpya ya Rais William Ruto ilipochukua usukani.

Serikali ya Kaunti ya Wajir ni moja kati ya kaunti zinazoongoza kwa malimbikizi ya madeni ambayo yamefikia zaidi ya Sh7.4 bilioni tangu mwisho wa bajeti iliyokamilika mnamo Juni 30, 2022.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Seneti inayosimamia Hesabu za Serikali, Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi alifichua kuwa ameanzisha uchunguzi kuhusiana na kiasi kikubwa cha madeni aliyorithi kutoka kwa mtangulizi wake.

Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Kaunti ya Homa Bay, Moses Kajwang ilielezwa kuwa huenda wafanyakazi au maafisa wa Kamati ya Makabidhiano walipachika bili bandia zilizosababisha malimbikizo ya madeni ya kaunti hiyo kuongezeka hadi Sh5.5bilioni.

“Ikiwa ukaguzi wa hesabu za serikali ulifanyika Juni 30 na deni lilikuwa Sh1 bilioni, uchaguzi ukafanyika Agosti, na magavana wakaapishwa katikati mwa Agosti, ilikuwaje nikapokea ripoti ya Sh5.5 bilioni kama malimbikizo ya madeni? Inamaanisha kuwa ama ripoti ya afisi ya Kamati ya Makabidhiano ina dosari au mchakato wa ukaguzi,” alisema Gavana.

Huku akifichua kuwa tayari serikali yake imeshtakiwa na miungano ya wafanyakazi, Bw Abdullahi alisema kuwa, alipochukua usukani, alipata deni la Sh1.5bilioni la ada za wafanyakazi ambazo hazijalipwa.

“Wajir ina tatizo sugu la malimbikizi ya madeni. Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Fedha iliyotolewa Juni 2022 ilionyesha kuwa deni la kaunti lilikuwa takriban Sh1 bilioni. Nilipochukua usukani deni hilo lilikuwa limefika Sh5.5bilioni na tangu hapo wanakandarasi wamekuwa wakiwasilisha nakala ambapo bili zimefikia Sh1.9bilioni,” alisema.

“Tumepelekwa kortini na miungano ya wafanyakazi kwa kukosa kulipa ada zinazokatwa wafanyakazi ikiwemo pesa za uzeeni, marupurupu, ada za vyama vya ushirika na mikopo ya waajiriwa. Tutabuni mbinu za kutoa malipo hayo.”

Tangu mfumo wa ugatuzi ulipoanzishwa mnamo 2013, Kaunti ya Wajir imekuwa na magavana wanne.

Bw Abdullahi (gavana wa sasa) alikuwa gavana wa kwanza kaunti hiyo akifuatiwa na Bw Mohamed Abdi aliyetimuliwa na nafasi yake kutwaliwa na aliyekuwa gavana Ali Muktar.

Seneti sasa imeagiza Tume ya Kukabiliana na Ufisadi (EACC) kuanzisha uchunguzi kuhusiana na Sh1.5 bilioni pesa zilizokatwa wafanyakazi lakini hazikulipwa katika Kaunti ya Wajir.

Wakiongozwa na Seneta Kajwang’, waundasheria hao sasa wanamtaka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madeni yote ambayo bado hayajalipwa huku suala la ada za kisheria likipatiwa kipaumbele.

Seneta wa Nandi Samson Cherargei alitaja deni la Sh1.5 bilioni kama “kupora umma hadharani” akisisitiza kwamba wahusika ni sharti wafungwe jela.

“Haifai kwa Wajir kuwa na deni linalotoshana na Nairobi. Wakazi wa Wajir wanahitaji kulindwa,” alisema Seneta wa Busia, Okiya Omtatah.

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto aongoza mkutano wa kundi la Wabunge na Maseneta...

Vihiga Queens waelekeza macho yote kwa CECAFA

T L