• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 11:50 AM
Mswada wa vitisho

Mswada wa vitisho

NA BENSON MATHEKA

RAIS William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua, wamezua vitisho kwa wale wanaopinga Mswada wa Fedha wa 2023, ambao unalenga kuongeza mzigo wa ushuru kwa Wakenya ikiwa ni pamoja na wafanyakazi kukatwa asilimia 3 ya mshahara wao kuchangia Hazina ya Nyumba.

Bunge la Kitaifa limeratibiwa kujadili Mswada tata wa Fedha 2023 wiki hii, na Rais William Ruto ametumia vitisho kuwashinikiza wabunge kuupitisha.

Kiongozi wa Nchi na Naibu wake, wamevuka mipaka wakiwaonya wabunge watakaokataa Mswada huo kusahau miradi ya maendeleo katika maeneo bunge yao.

Hii ni licha ya kuwa bunge linapaswa kuwa huru katika kufanya maamuzi yake.

“Nasubiri kuona wabunge ambao wataenda kinyume na mpango wa serikali wa kuwapa wapiga kura wao ajira. Tunataka kuona na kujua wanaoenda kinyume na Mswada huu wa Fedha,” Rais alisema mjini Narok wakati wa ibada ya kutoa shukrani.

“Nimesikia baadhi ya watu wakisema, wanasubiri kuona wabunge ambao watapiga kura ili Mswada huo upite, lakini nasubiri vile vile kuona wabunge watakaopiga kura kuupinga Mswada wa Sheria ya Fedha unaolenga kuhakikisha vijana wanapata ajira. Nasubiri kuona wanaopinga mpango unaowapa uwezo vijana waliowapigia kura,” rais aliongeza.

Naibu Rais Rigathi Gachagua pia amewaonya viongozi wanaopinga Mswada huo kutotarajia miradi ya maendeleo katika maeneo bunge yao.

Bw Gachagua aliwaambia Wabunge wanaopinga Mswada wa Fedha wa 2023, wasitarajie pesa zozote za miradi ya miundomsingi katika maeneo bunge yao.

Kulingana na Bw Gachagua, serikali inategemea Mswada huo kuongeza mapato, na wabunge wanapaswa kuunga mkono kikamilifu ikiwa wanatarajia kupata fedha za maendeleo.

“Baadhi yenu viongozi mnadanganya Wakenya, lakini fahamuni kwamba ikiwa mbunge wenu anapinga Mswada wa Fedha, hawafai kuuliza barabara,” alisema.

Akizungumza akiwa Kitui Jumamosi iliyopita, naibu rais alisema hazina hiyo itatumika kujenga shule, kukarabati barabara na kuweka miundomsingi mingine ingawa inalenga kuwajengea Wakenya nyumba za bei nafuu.

“Mimi ni mtu ninayesema ukweli; lazima watu watoe kodi kugharamia matumizi ya kawaida, kuna wito wa kuajiri walimu zaidi, nani atalipia hili? Siwezi kulipia kwa mshahara wangu wa Sh1 milioni, fedha hizo zitapatikana kutoka kwa wananchi,” alisema.

Mnamo Jumatatu, Bw Gachagua alitoa onyo jingine kwa magavana kutopinga mswada huo. Akihutubia wanahabari baada ya kuongoza mkutano wa Baraza la Bajeti na Uchumi kati ya viwango viwili vya serikali (IBEC), Bw Gachagua aliwaonya magavana wasiunge juhudi za kupinga Mswada huo.

“Tuko katika hali moja na mkikosa kuunga mkono Mswada huo hatutakuwa na pesa za kuwasaidia,” Gachagua alionya.

Serikali pia imeonya upinzani na mashirika ya kiraia kwamba, haitaruhusu maandamano huku viongozi wa Azimio wakidokeza kuwaita wafuasi wao kuandamana.

Mnamo Jumatatu, kiongozi wa Azimio Raila Odinga, aliipa serikali siku mbili kuondoa vipengee vyenye utata katika Mswada huo, akisema kuwa atatoa tangazo hivi karibuni.

Jana Jumanne, polisi walitawanya kundi la wanaharakati waliokuwa wakiandamana kwa amani kuelekea bungeni kupinga Mswada huo.

  • Tags

You can share this post!

Mikakati ya Azimio kuzima Mswada wa Fedha 2023 imeiva

Maombi ya kitaifa: Mbunge Silvanus Osoro ni gwiji katika...

T L