• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
Muturi awaita wabunge tena kujadili mswada tata wa vyama vya kisiasa

Muturi awaita wabunge tena kujadili mswada tata wa vyama vya kisiasa

Na CHARLES WASONGA

SIKU moja baada ya wabunge wandani wa Naibu Rais William Ruto kufaulu kuchelewesha kupitishwa kwa Mswada tata wa marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ameitisha kikao kingine maalum cha kushughulikia mswada huo.

Kulingana na tangazo alilotoa Alhamisi jioni Bw Muturi amewaita wabunge kufika bungeni mnamo Jumatano, Desemba 29, 2021 kwa ajili ya kujadili mswada huo katika hatua ya tatu (Third Reading). “Kulingana na sheria za bunge nambari 29 (1) kuhusu vikao maalum, nimekubali ombi la kiongozi wa wengi kwamba kikao maalum cha bunge la kitaifa kifanyike Desemba 29, 2021”

Kwa hivyo wabunge na umma kwa ujumbe wanajulishwa kwamba Jumatano, Desemba 29, 2021 imeteuliwa kuwa siku ya kufanyika kwa kikao maalum cha bunge la kitaifa. Kikao hicho kitafanyika katika ukumbi wa bunge hili kuanzia saa nne asubuhi (10 am) na saa nane na nusu alasiri (2.30 pm) kwa ajili ya, miongoni mwa shughuli zingine, kujadili mswada wa marekebisho ya sheria za vyama vya kisiasa katika hatua ya tatu,” akasema Bw Muturi katika ilani.

Spika huyo aliongeza kuwa huenda bunge hili likafanya kikao cha jioni au usiku ikiwa shughuli hiyo haitakamilishwa katika muda wa kawaida. Bw Muturi amewataka wabunge wote ambao waliwasilisha jumla ya marekebisho 17 kwa mswada huo kufika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) mnamo Jumanne Desemba 28, 2021 kwa kikao cha kuyaoanisha marekebisho hayo.

Ni marekebisho hayo, mengi yakiwasilishwa na wabunge wanaoegemea mrengo wa Tangatanga, ambayo yalichangia Naibu Spika Moses Cheboi kusitisha kikao maalum cha Jumatano, Desemba 22,2021 kabla ya mswada huo kushughulikiwa kikamilifu.Wabunge hao walipinga vikali mswada huo ambao unalenga kuipa miungano ya vyama vya kisiasa kama vyama, sifa sawa na vyama vya kisiasa.

Walidai hiyo ni njama ya kuhalalisha vuguvugu la Azimio la Umoja ambalo kiongozi wa ODM Raila Odinga analenga kuligeuza kuwa muungano ambao utadhamini wagombeaji katika uchaguzi mkuu wa 2022. Bw Odinga, anapania kuwani urais kwa tiketi ya muungano huo ambao unatarajiwa kujumuisha chama tawala cha Jubilee na vyama vingine vyenye maoni sawa na Azimio la Umoja.

Wabunge wa tangatanga pia wanapinga mswada huo kwa misingi kuwa unapendekeza kuwa stakabadhi za kubuni miungano kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao ziwasilishwe kwa afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa Anne Nderitu miezi sita kabla ya uchaguzi mkuu.

Wanafasiri pendekezo hilo kama njama ya kuwalazimisha kuchukua misimamo ya kisiasa mapema , hali ambayo inaashiria kuwa watalazimika kujiuzulu rasmi kutoka Jubilee na hivyo kupoteza viti vyao miezi sita kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Wabunge hao ambao wameapa kutetea viti vyao au kuwania vingine kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) pia wanadai mswada huo umeipa afisi ya Msajili Mkuu wa Vyama vya Kisiasa mamlaka makubwa zaidi kiasi kwamba “anaweza kuondoa jina la mtu kutoka orodha ya wanachama wa chama fulani.”

Ubabe kati ya wabunge wa mrengo wa Dkt Ruto na wale wa mrengo wa handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga, unatarajiwa kushuhudiwa tena bungeni siku hiyo, Jumatano, Desemba 29, 2021.

You can share this post!

Kesi ya ukwepaji ushuru dhidi ya Bilionea Kariuki...

Ndondi kutua mashinani kwa fujo hatimaye

T L